BARAZA la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limesema ushiriki wa Watanzania watatu katika Tuzo za Hamad mwaka huu kwa kutafsiri kitabu cha Kiswahili kwenda kwenye Lugha ya Kiarabu kimeiongezea hadhi Kiswahili.
Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi alisema hii ni mara ya kwanza kwa Lugha ya Kiswahili kuingizwa kwenye ushindani wa tuzo hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 2015. Mushi aliwataja Watanzania wanaoshiriki tuzo hiyo kuwa ni Shawar Marinda, Daud Amir na Maisara Simai.
“Kupitia mfumo ule, lazima utafsiri kitabu ambacho toka kuchapishwa kisizidi miaka mitano na unaweza kutafsiri kutoka Kiswahili kwenda Kiarabu na kutoka Kiarabu kwenda Kiswahili, kwa hiyo washiriki wengi hapa wametafsiri kutoka Kiswahili kwenda Kiarabu,” alisema.
Awali, Mushi alisema kuna tuzo mbili za kushindaniwa ya kwanza ikiwa ni tuzo ya tafsiri kutoka Lugha ya Kiarabu kwenda Lugha ya Kiswahili na tuzo ya tafsiri kutoka Lugha ya Kiswahili kwenda Lugha ya Kiarabu, ambayo kila tuzo ni Dola za Marekani 100,000 (Sh 233,141,805).
“Tunawapa kongole kwa kuthubutu kushiriki na kwa kuwa hii ni mara ya kwanza Kiswahili kuingizwa kwenye tuzo hizi za Hamad, kama tungekosa mshiriki ingeonekana labda lugha hii haina watu wengi au wapenzi, lakini kwa kushiriki kwao imeonesha kuwa kuna watu tayari wanajua Kiarabu na wanajua Kiswahili,” alisema Mushi.
Kwa mujibu wa Mushi, hata kama Watanzania hao hawatashinda jambo hilo linaweza kuwavutia waandaaji kuwaingiza kwenye shughuli nyingine zaidi. Alisema pamoja na kwamba wakishinda watapata fedha, jambo la msingi ni uthubutu wao wa kushiriki unaoonesha kuwa Lugha ya Kiswahili ina huo uwezo wa kushiriki.
Alisema tuzo hizo zinatolewa na Taasisi ya Hamad Award for Translation and International Understanding ya Qatar na washindi hukabidhiwa tuzo zao nchini humo.
Alisema tuzo hizo zinatolewa kutambua na kuthamini mchango wa wafasiri na jukumu lao la kuunganisha watu wa mataifa duniani, kuhimiza watu binafsi, wachapaji, asasi na taasisi za Kiarabu na kimataifa kuongeza jitihada zaidi katika tafsiri zenye ubora na ubunifu kutoka na kwenda kwenye Kiarabu.
Alilitaja lengo lingine la tuzo hizo ni kuboresha ubora tafsiri zinazofanywa kutoka au kwenda Kiarabu kwa kuzingatia ubora wa hali ya juu, usahihi na maadili kitaalamu.