Watatu kortini wakidaiwa kumuua mfanyabiashara

JESHI la Polisi limewakamata watu watatu na kuwapandisha kizimbani wakidaiwa kumuua mfanyabiashara wa mazao ya nyuki.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Demotrio Nyakunga waliosomewa shitaka la mauaji ni Feruz Abdalah Feruzi, Masumbuko Said Ramadhan na Tumba Shabani.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Joseph Mwambwalulu ulidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Julai 14, mwaka jana.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio saa nne asubuhi eneo la Kazuge Kata ya Mpera Manispaa ya Tabora, washitakiwa walimuua kwa kumpiga risasi Mohamed Mustapha Ngedela akiwa nyumbani kwake.

Mwambwalulu alidai kuwa baada ya kutenda kosa hilo walitoroka kwa pikipiki lakini polisi waliwakamata na kuwashitaki.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na imepangwa kutajwa Februari 14, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button