SERIKALI ya Uganda imesema kuwa imewakamata watu watatu wanaohusishwa na shambulio dhidi ya Shule ya Sekondari Lhubiriha siku ya Ijumaa, ambako karibu watu 40 walipoteza maisha wengi wao wakiwa wanafunzi.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunafuatia msako mkali ambao unaoendelea kufanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika Mji wa Mpondwe uliopo Magharibi mwa nchi hiyo.
Mkuu wa Wilaya Joe Walusimbi, amesema kukamatwa kwa watu hao kumefanikishwa na taarifa iliyotolewa na wakazi wa eneo hilo.
Lakini aliongeza kuwa jeshi la Uganda bado linaendelea kuwasaka wanamgambo wa Kiislamu ambao wamekuwa wakilaumiwa kwa shambulio hilo, huku wakiripotiwa kukimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).