Watendaji Kigoma wawekwa kikaangoni

KIGOMA: MKUU wa wilaya Kigoma Salum Kali amekemea utendaji kazi wa wakuu wa idara na wataalam wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kushindwa kutumia weledi wao katika kutekeleza majukumu yao na kuisababisha halmashauri hiyo migogoro na wananchi inayokwamisha maendeleo.

Kali ameyasema hayo  katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la halamshauri hiyo ambapo zimeibuka hoja mbalimbali za kiutendaji zilizoshindwa kutolewa maelezo ya kutosha na watalaam ikionyesha wataalam hao kushindwa kutumia nafasi zao kusimamia hoja hizo.

Miongoni mwa hoja ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu ni pamoja na migogoro ya ardhi ambapo watendaji idara ya ardhi wanashutumiwa kuuza viwanja na kutoa hati katika maeneo ambayo yamechangia kuwepo kwa migogoro isiyoisha.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa amekuwa akitumia muda mwingi kushughulikia migogoro mbalimbali ya kiutendaji na migogoro ya ardhi ambayo iko chini ya wakuu wa idara na watalaam jambo ambalo linamnyima muda wa kutosha kwenda kwa wananchi kushiriki utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Awali Diwani wa kata ya Rubuga,Omari Gindi aliwashilisha hoja binafsi ya malalamiko ya uuzwaji wa viwanja akitoa mfano wa kiwanja namba 170 ambacho kiliuzwa na wataalam wa idara ya ardhi bila kufuata taratibu huku Diwani wa kata ya Buhanda,Kilahumba Gilbert akiwasilisha malalamiko ya mgogoro wa kiwanja cha mtu mmoja aliyefariki ambaye kiwanja chake kimeuzwa bila kufuata taratibu baada ya kufariki.

Aidha Diwani wa kata ya Kibirizi, Ramadhani Ruhiso aliwasilisha hoja maalum ya kuuzwa kwa eneo la halmashauri jirani na eneo la Bandari Kavu Katosho huku Afisa mipango miji akitoa taarifa za uongo kuhusu umiliki wa halmashauri wa eneo hilo na kuomba baraza likae kama kamati kujadili hoja hiyo.

Kufuatia hoja hizo baraza lilijigeuza kama kamati na kujadili mambo mbalimbali ambapo Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji,Baraka Lupoli  alitoa taarifa ya kamati ambayo imefikia maamuzi ya Kumvua madaraka Kaimu Afisa mipango miji wa halmashauri hiyo, Zabron Magesa  sambamba na kuitaka serikali kumuondoa mtumishi huyo kwenye halmashauri hiyo.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button