Watendaji Nanyamba wafundwa

WATENDAJI wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara wametakiwa kila mmoja kwa nafasi yake awajibike ipasavyo kuhakikisha halmashauri hiyo inapiga hatua kimaendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mwinyi Ahmed amesema wanayo kazi ya ziada hasa kwa kuzingatia shughuli, majukumu yao wanayotakiwa kuyafanya juu ya usimamizi wa maendeleo ya halmashauri.

Hayo yamesemwa leo Februari 8, 2024 wakati wa kikao cha siku mbili cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kuhusu kupitia taarifa za shughuli za maendeleo katika kata mbalimbali kwenye mji huo, robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Advertisement

‘’Tubadilike, zama zimebadilika tuache kufanya kazi kwa mazowea badala yake kila mmoja kwa nafasi yake awajibike tuna kazi ya ziada hasa ya mazingatio ya shughuli zetu tunazotakiwa kuzifanya’’amesema Mwinyi

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jamali Kapende ameendelea kuwasisitiza watendaji hao kuwa  waendelee kufanya kazi kwa niaba ya wananchi kwani linaloweza kutekelezwa, kufanyika sasa lifanyike ili kuleta tija ya maendeleo katika mji huo.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Prosper Kisinini amesema maelekezo yote yaliyotolewa katika kikoa hicho yamepokelewa na kuahidi kuyafanyia kazi.

Mbali na hilo, kata ya Nanyamba ni moja kati ya kata 17 zilizopo kwenye halmashauri hiyo iliyofanikiwa kuvuka lengo walilojiwekea katika ukusanyaji mapato kwenye robo hiyo  ambayo ni zaidi ya Sh milioni 8 sawa na asilimia 112.8.

Hata hivyo lengo lilikuwa ni kukusanya  zaidi ya Sh milioni 7 kwenye robo  huku lengo kuu likiwa kukusanya Sh milioni 30 kwa mwaka huo wa fedha 2023/24.