“Watendaji wangu acheni kuchepusha barabara”

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuacha mpango wa kutaka kuchepusha barabara kuu eneo la Dumila kwa kupitisha eneo la juu la mto kilometa 10 kutoka daraja lililopo na kujenga daraja jingine kwenye njia iyakayochepushwa .

Kwa kuzingatia maoni ya wananchi wa Dumila ameutaka wakala huo kuchukua hatua za kuliimalisha zaidi daraja hilo kwa kufanya usanifu wa kina kwani tayari eneo hilo kuna uwekezaji mkubwa wa watu na huduma za kijamii zikiwemo shule na vituo vya afya katika mji huo.

Waziri Bashungwa alisitiza mpango huo baada ya kupata maoni ya wananchi wa Dumila pamoja na mbunge wa Jimbo la Kilosa ,Profesa  Palamagamba Kabudi wakati alipokagua daraja hilo.

Mara kadhaa daraja hilo limekuwa tishio kwa wasafiri wa barabara ya Dar es Salaam – Morogoro- Dodoma na mikoa mingine kwa sababu ya daraja hilo ujaa mchanga.

Bashungwa alisema ili kutatua changamoto hiyo Serikali kupitia wataalam wa Wizara ya Ujenzi walifikia uamuzi wa kuchepusha barabara hiyo kupita eneo la juu la mto huo kilometa  10 kutoka daraja lililopo sasa na kujenga daraja jingine.

“Nimesikiliza maoni ya wananchi, serikali ya mkoa na mbunge wa jimbo hili la Kilosa sasa nimeagiza watendaji wangu waache kuchepusha barabara hii na daraja hili libaki  mahali lilipo badala yake , wafanye usanifu wa kina  ambao utaweza kuliimalisha zaidi daraja hili kwa kuwa tayari  hapa mji wa Dumila kuna uwekezaji mkubwa wa watu na Serikali. “alisema Bashungwa.

Katika hatua nyingine waziri huyo ameeleza zitafutwe fedha zitakazotumika kupanua barabara ya mjini Morogoro kutoka eneo la Kingolwila hadi Kihonda pamoja na Msamvu hadi Mafiga ili kuondoa changamoto ya msongamano wa magari uliopo sasa.

“ Nikuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba kuanza kufanya tahmnini ya fedha zinazohitajika katika upanuzi wa barabara hizo  ili kuanza kutekeleza wake kwa ajili ya kuondoa msongamano wa magari.

“ alisisitiza Bashungwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameendelea kuwaomba watu wa Dumila kuwa wavumilivu kutokana na kadhia ya maji yanayotokana na mto kuacha njia yake na kumwaga maji kwenye  makazi ya watu.

“Serikali ya awamu ya sita iko mbioni kushughulikia changamoto hizi “ alisema Malima .

Malima alimuomba Waziri wa Ujenzi wakishirikiana na Wizara ya Kilimo kuona uwezekano wa kujengwa mabwawa juu ya mto huo ili kupunguza kasi ya maji hayo na kutumika kwenye kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu.

Habari Zifananazo

Back to top button