Watengeneza dawa asili ya kusindika ngozi kuondoa kemikali

TAASISI ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imebuni dawa ya asili ya kusindika ngozi ambayo itasaidia kuondoa matumizi na utegemezi wa kemikali kutoka nje.

Haya yameelezwa na Mhadhiri Dk Cecilia China alipozungumza na HabariLEO wakati wa maonesho ya Wiki ya Ubunifu yaliyofanyika jijini hapa.

Alisema ubunifu wa dawa hiyo ambayo imetengenezwa kwa kutumia mitishamba itasaidia kutatua tatizo la upatikanaji wa kemikali za kusindika ngozi.

Advertisement

“Kwa sasa hapa nchini hatuna kiwanda cha kuzalisha kemikali za kusindika ngozi, tunaingiza hizi dawa kutoka nje na wajasiriamali wengi ambao wanasindika ngozi na ambao ni wengi hawana uwezo wa kumudu zile dawa kwa sababu viwanda vyao vidogo,” alisema.

Alisema pia matumizi ya dawa isiyo na kemikali itasaidia katika utunzaji mazingira. Dk China alisema ubunifu huo aliouanza akiwa anasoma shahada yake ya PhD, ulipata ushindi wa kwanza katika kundi la vyuo vikuu wakati wa Makisatu ya mwaka 2020.

“Hiyo ilinipa fursa ya kufadhiliwa na Costech kwa ajili ya kuendelea, fedha nilizopewa ziliwezesha kubuni mtambo wa kutengeneza dawa na kuilinda kisheria.” Alisema kupitia mradi wa Kongani Bunifu, Costech ilimfadhili ili kuhamisha teknolojia kwa kikundi cha wasindika ngozi chenye wanachama 15 kilichomo Usangi mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Dk China alisema kwa sasa wana mpango wa kusajili kampuni ya jamii ambayo itahusika kutengeneza dawa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo, kufundisha namna ya kutumia na kutafutiwa masoko.

Naye Ofisa Usimamizi wa tafiti kutoka taasisi hiyo, Okuli Andrea alisema taasisi ya Nelson Mandela imejikita katika kutoa shahada za uzamili na uzamivu na kufanya tafiti mbalimbali za kutatua matatizo mbalimbali katika jamii.

“Katika maonesho haya ya Wiki ya Ubunifu mwaka 2023, tumekuja na bunifu mbalimbali ambazo zinatatua changamoto katika jamii ambazo ni bidhaa za ngozi zisizotumia kemikali, ngwara yenye virutubisho, vyakula lishe na mtambo wa kusafisha maji na bidhaa nyingine mbalimbali,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *