Watengeneza mfumo kudhibiti hali ya hewa mashambani

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimetengeneza mfumo wa kusaidia kudhibiti hali ya hewa ndani ya mashamba, ili uendane na zao husika lengo likiwa ni kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa faida.

Mtafiti Paschal Magambo kutoka UDOM ambaye ametengeneza mfumo huo uliopo katika umbo la ‘Green House’,  amesema una uwezo wa kuzalisha unyevunyevu uhaohitajika katika eneo la shamba, vile vile kuzalisha joto endapo baridi imezidi.

Amesema  matumizi ya green house kwa muda mrefu yamekuwa yakiwapa watu  mavuno madogo tofauti na matarajio yao, hali iliyosababisha wasipate faida waliyokuwa wakiitegemea wakati wanaanza kulima.

Advertisement

“Green house nyingi zilizopo sasa zimekuwa zikifanya kazi ya kuzuia wadudu pekee, lakini hazina uwezo wa kudhibiti hali ya hewa ndani ya shamba husika.

“Sasa sisi tumekuja na mfumo ambao utawawezesha wakulima kulima kwa kujiamini na kutegemea matokeo asilimia 100, mtu akishakuwa na mfumo huu utamsaidia kulima bila kujali hali ya hewa na akafanikiwa,” amesema.

Amesema hali hiyo ni kutokana na mfumo huo kuwekewa uwezo wa kuzalisha unyevu unaohitajika katika zao husika na joto linalohitajika katika zao husika, hivyo kumfanya hata asiyekuwa na elimu ya kilimo kulima bila tatizo lolote.

“Hapa katika remote yetu kuna mazao aina tofauti ikiwa unalima tikiti maji utabonyeza kitufe chake na baada ya hapo mfumo utakuambia joto linalohitajika ni kiasi gani na unyevu kiasi gani na lililopo ni kiasi gani, hivyo utajua kama unatakiwa kuongeza au kupunguza.

“Kuna baadhi ya mazao ambayo hayahitaji joto kali au baridi kali, mfumo huu utasaidia kuzalisha unyevu ambao utakuwa unahitajika kwa zao husika, ambayo pia itakuwa inashusha joto na kufanya mmea ustawi vizuri,” amesema.

Mkulima kutoka Njombe, Anna Mwaso ambaye ametembelea Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba amesema bunifu zinazolenga kilimo ni vyema ziwezeshwe kwa haraka, ili zilete manufaa.

“Unajua wengi wakiambiwa green house wanajua ni kuweka tu lile net basi, wakati mmea unahitaji vitu vingi ili ukue na kukupa matokeo tarajiwa ikiwemo hali ya hewa ambayo ni muhimu kuliko kitu chochote,” amesema.

 

2 comments

Comments are closed.