Watetezi wa uhai Afrika kujadili mimba za maabara

VIONGOZI wa mashirika ya kutetea uhai wanaoshirikiana na shirika la kimataifa la kutetea uhai Human Life International (HLI) katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika na nchi zinazozungumza Kiingereza, wanatarajia kukutana Kampala, Uganda katika kongamano kuhusu heshima ya uhai wa mwanadamu katika asili yake na hadhi ya uzazi sambamba na uhalali wa kimaadili wa mimba katika maabara za kisayansi.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitakazoshiriki kongamano hilo la Mei 29 hadi Juni 4, mwaka huu katika Kituo cha Emaus kilichopo nje kidogo ya Jiji la Kampala ni Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya na wenyeji Uganda.

Nchi nyingine zitakazowakilishwa na viongozi wa mashirika ya kutetea uhai ni Lesotho, Namibia, Nigeria, Zimbabwe, Zambia na Malawi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa HLI- Afrika kwa Nchi Zinazozungumza Kiingereza, Emil Hagamu mada katika kongamano hilo zitarejea waraka unaohusu mafundisho ya Kanisa Katoliki uliotolewa na Idara ya Mafundisho ya Imani ya Vatikano mwaka 1987 ukijibu hoja za maadili ya kibayolojia kuhusu majaribio mbalimbali katika mwili wa mwanadamu yananayofanywa na wanasayansi.

Mwaka jana kongamano hilo lilifanyika Tanzania na kujadili Nafasi ya Familia ya Kikristo katika Dunia ya Leo.

“Kongamano hilo ni muhimu sana kwani tunaona jinsi binadamu anavyodhalilishwa na kutumika kama bidhaa katika majaribio mbalimbali ya kisayansi…,” alisema na kuongeza:

“Maendeleo ya kisayansi daima yanapaswa kuzingatia kulinda na kuheshimu uhai wa binadamu na namna uhai huo unavyopasishwa katika maisha ya ndoa.”

Hagamu alisema waraka huo unakwenda sambamba na waraka mwingine uitwao “Dignitas Personae” wa Juni 20, 2008 unaoendeleza mafundisho ya kanisa katika masuala ya maendeleo ya sayansi katika ‘biolojia-maadili’ ambayo hayakufundishwa katika Waraka wa Donum Vitae.

“Katika nyaraka zote mbili, mafundisho yameelezwa kwa ufasaha kuwa uhai wa kila binadamu unapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa kwa sababu binadamu ni kiumbe pekee duniani ambacho uumbaji wake ulidhaminiwa na Mungu mwenyewe na roho yake imetokana na Mungu mwenyewe, uwepo wa binadamu unadhihirisha mfano wa Mungu mwenyewe,” alisema.

Alizitaja mada zitakazojadiliwa katika kongamano hilo kuwa ni pamoja na; Je, mimba ipewe heshima tukichukulia hadhi yake na utu wake? Je, ni halali kimaadili kufanya uchunguzi katika mimba?  Je, kanuni gani ya kimaadili itumike kuruhusu uchunguzi wa mimba zinazopatikana kwa njia ya teknolojia?’

Mada nyingine ni: Kwa nini mimba lazima itungwe katika ndoa pekee? ‘Je, inaruhusiwa kimaadili kupandikiza mbegu kwa wanawake wenye shida ya uzazi? Na je, kimaadili ni sahihi kutunza mimba katika majokofu na kisha kutumia kwa malengo mengine ya kisayansi?’

Habari Zifananazo

Back to top button