WAHITIMU wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (OUT), wameombwa kutoa mrejesho wa kile walichofundishwa kama kinaendana na soko la ajira nchini ili kama hakiendani kibadilishwe.
Aidha waajiri nao wametakiwa kutoa mrejesho wa wahitimu wa OUT kwa chuo hicho ili kukiwezesha kufanya maboresho ya mitaala yanayoenda na wakati wa sasa.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda ametoa ombi hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho ya mitaala wanayoyafanya hivi sasa chuoni hapo.
Profesa Bisanda amesema kupitia wahitimu hao na waajiri wao wataweza kutathimini upya mitaala kwa kuangalia elimu wanayoitoa kama inalenga mahitaji ya sasa hivi na sio kama wanafundisha kimazoea.
” Lengo ni kupata taarifa halisi tuwaone wale wahitimu walipoenda kufanya kazi watuambie upungufu wa elimu tuliyowapa kama upo.
” Lakini pia waeleze sehemu gani tunaweza kuboresha mitaala yetu ili wahitimu watakaohitimu wawe na weledi na waweze kuingia vizuri katika kuboresha uchumi wa nchi ,” amesema.
Profesa Bisanda amesema lengo ni kumsaidia mwananchi wa kawaida aweze kutumia rasilimali za nchi zilizopo vizuri na aweze kuchangia pato la taifa na pato lake binafsi.
Amesema katika kufanya tathmini hiyo ni lazima wapate taarifa za mitaala waliyokuwa wanaitoa .
” Tutamuuliza mhitimu ulisoma kozi gani, aliona imemsaidia nini , ina upungufu upi ili tusaidie tunapoanza kuchambua ile mitaala, tuiboreshe” amesema.
Amesema kama kuna mitaala itaonekana haina manufaa yoyote itaondolewa kwa kuwa haisaidii.
” Kwa hiyo mitaala tunayoitoa, kozi tunazotoa ilete mahitaji halisi ya jamii na jumuiya yetu,” amesema.
Mabadiliko ya mitaala hiyo yanafanyika kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaotekelezwa na serikali katika vyuo vyake vyote nchini.