Watoa ushauri mikopo elimu ya juu

WADAU wa elimu nchini wamesema Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapaswa kutenda haki na kuzingatia vigezo ili wanaostahili waipate na wasiostahili wasipate.

Walisema hayo wakati wakizungumzia uamuzi wa serikali kuunda timu ya kuchunguza mchakato wa utoaji wa mikopo kwa ajili ya wanafunzi hao ili kubaini changamoto na kutoa ushauri.

Hivi karibuni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema serikali inakaribisha taarifa za wananchi kwa ajili ya uchunguzi unaoendelea kuhusu mchakato wa kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Advertisement

Profesa Mkenda alisema Dar es Salaam kuwa timu ya watu watatu inayoongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro (Utawala), Profesa Allan Mushi inaendelea kuchunguza mikopo hiyo.

Wengine kwenye timu hiyo ni mtaalamu wa takwimu kutoka Zanzibar, Idd Makame na Dk Martin Chegeni.

Profesa Mkenda alisema timu hiyo ina kazi ya kuangalia taratibu zilizotumika kutoa mikopo kwa angalau miaka mitano iliyopita.

Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Kongwa mkoani Dodoma, Noah Magomba aliipongeza serikali kwa kuamua kuchunguza mchakato wa kutoa mikopo na kwamba utasaidia kuboresha mikopo.

“Katika kuboresha mchakato wa utoaji wa mikopo, vigezo vizingatiwe ili mikopo isitolewe kwa watu wenye uwezo, HESLB wawekwe watu wenye uzalendo wasiotenda kazi kwa upendeleo au kujuana kwa sababu waombaji hawana shida tatizo ni kwa watoaji,” alisema Magomba.

Mkuu wa Shule ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopo Dar es Salaam, Sylvanus Balagulana alisema serikali imefanya uamuzi wa busara kuchunguza mchakato wa mikopo hiyo kwa kuwa itaziba mianya ya rushwa na upendeleo kama upo.

“Ili kuboresha utoaji huo wa mikopo, vigezo wanavyoweka vizingatiwe ikiwemo kuzingatia hali ya mtu kusoma tangu akiwa chini kabisa,” alisema Balagulana.

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Katoliki Mwenge mkoani Kilimanjaro (MWECAU), Dk Peter Siamoo aliunga mkono uamuzi wa serikali wa kuchunguza mchakato wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha hizo ni kodi za wananchi.

Dk Siamoo alisema kwenye nchi yenye idadi ya watu wengi kama Tanzania, si rahisi kukosa watu wachache wanaoweza kutumia fursa ya mikopo hiyo kujinufaisha.

“Mikopo hii inasaidia vijana wetu ambao ni Watanzania kupata elimu ili baadaye waje kulitumikia Taifa lao. Kwa hiyo lengo la serikali ni kujiridhisha kama kodi ya Watanzania haiendi kwenye mikono isiyo halali,” alisema.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo alisema uamuzi huo wa serikali ni muhimu kwa kuwa ufuatiliaji huo utasaidia kubaini utekelezaji na kupima matokeo ya utoaji wa mikopo hiyo kama ulikuwa chanya au hasi.

“Timu hiyo ina nafasi nzuri ya kubaini ukweli na kuja na majawabu yatakayosaidia si tu kuona nini kilifanyika bali pia kuona kitu gani kiboreshwe ili kuondoa malalamiko,” alisema Mwalongo.

 

1 comments

Comments are closed.