MANYARA: BENKI ya Biashara ya Mkombozi imetoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 7.7, ikiwa na lengo la kuwashika mkono waathirika wa maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang yaliyotokea Desemba 2023 kwenye mji mdogo wa Katesh.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Respige Kimati amesema benki yao ni ya wananchi ipo mbele kuhakikisha inatoa huduma mbalimbali za kibenki nchini na katika nyakati kama hizo wamekuwa wakiungana na Watanzania kuwashika mkono.
”Tunafurahi sana siku ya leo kukabidhi vifaa hivi kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hii ya Hanang kama msaada wetu, ili kwa utaratibu mliojiwekea uweze kuwafikia wale wote wananchi waliopata na maafa,”amesema na kuongeza:
”Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na maafa, ambao walipoteza ndugu na jamaa zao, benki ya mkombozi inatazama na kushughulika na wateja wa aina zote, tumeweka kipaumbele kwa wateja wadogo wakiwemo wa vijijini na kujenga mtandao ambao utaimarisha utoaji wao wa huduma za kibenki,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja alishukuru uongozi wa benki hiyo kwa kuwapa pole waathirika na kuwapatia vifaa vya ujenzi vitakavyosaidia shughuli zinazoendelea kufanyika za ujenzi wa nyumba za waathirika hao.