Watoto 14, 000 wanazaliwa na Selimundu nchini

Serikali yatoa mwongozo

TAKWIMU zinaonyesha Watoto  11, 000 hadi 14, 000 14 wanazaliwa nchini wakiwa na changamoto ya selimundu (Sickle Cell)  huku asilimia saba ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinatokana na changamoto ya ugonjwa huo.

Hayo, yamesemwa leo Julai 12, 2023 na Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumani Nagu katika Kongamano la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu na uzinduzi wa jarida rasmi la Selimundu la Lancet.

Profesa Nagu amesema  “Hii ina maana kwamba kwa kila watoto elfu moja wanaozaliwa nchini Tanzania, watoto kumi na moja wana ugonjwa wa ‘Sickle Cell’ ”

Amesema takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya tano duniani kwa kuwa na wingi wa wagonjwa wa  Selimundu na kuwa ya tatu katika bara la Afrika.

Pia, amesema katika vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano ugonjwa wa Selimundu husababisha vifo  15,000 kila mwaka sawa na asilimia saba ya vifo vyote vya watoto.

Aidha, kutokana na changamoto hizo Prof. Nagu amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao umekua na athari kubwa katika jamii ikiwemo kutoa  muongozo wa matibabu ya selimundu  nchini.

Amesema, muongozo huo  unaainisha nyanja zote kuanzia kupunguza tatizo hilo kwa kufanya utambuzi wa watoto wachanga  na uhakika wa matibabu.

Aidha, muongozo huo unaelekeza kufanyika vipimo vya vinasaba kwa wachumba kabla ya kuoana ili kupunguza uwezekano wa kupata watoto wenye selimundu.

Alieleza kuwa muongozo huo unalenga kufanya utambuzi kwa watoto zaidi ya milioni mbili wanaozaliwa kila mwaka na kuhakikisha wanapata matibabu mapema ikiwemo chanjo, dawa za antibiotiki ili wasipate changamoto zitokanazo na selimundu.

Pia amesema,  muongozo huo utahakikisha kuwa watoa huduma wao wanajua namna bora ya kuwahudumia kwa usahihi wenye matatizo hayo hivyo, kuboresha matibabu ya watoto hao.

“Serikali inafanya jitihada kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuwatambua watoto mapema katika hospitali zote saba ikiwemo ya Taifa, Kanda na Rufaa za Mikoa ili kuhakikisha matibabu ya watoto yanakuwa mazuri na bora,” amesema  Prof. Nagu.

Kwa mujibu wa Prof. Nagu, watahakikisha dawa ambayo inabadilisha maisha ya watoto wenye selimundu ya Hydroxyurea  inapatikana Tanzania kwa kutengenezwa hapa nchini.

Amesema, dawa hiyo ikitengenezwa nchini itapunguza gharama na kuhakikisha inakuwepo muda wote badala ya kusubiri itoke nje ya nchi.

“Kwa sasa Bohari ya Dawa (MSD) inatoa dawa hiyo muda wote, serikali  imetenga fedha kwajili ya kununua dawa hii ambayo ipo kwenye miongozo ya dawa na kusaidia hospitali na vituo vya afya kuagiza.

“Nipende kuwakumbusha waganga wafawidhi wa hospitali kuhakikisha dawa hii inapatikana kwenye vituo vyote vya afya kwani ipo na inapatikana wakati wote.”Amesema

Kuhusu upandikizaji uloto, Profesa Nagu amesema matibabu hayo hupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo na hupatikana katika Hospitali za Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema gharama za matibabu hayo ni makubwa kwa sababu inahitaji kufanyika vipimo vingi na vikubwa ambavyo hupatikana ndani na nje ya nchi.

“Katika bajeti ya mwaka 2023/24 serikali imetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya upandikizaji na kwa sehemu kubwa itatumika kupandikiza uloto na figo,” amesema.

Alisisitiza kuwa wako tayari kufanya kazi na watafiti kuhakikisha zinajibu matatizo ya Watanzania.

Kwa upande wa Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha Muhas, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema  tafiti walizofanya zimechangia maboresho ya huduma za ugonjwa wa selimundu nchini ikiwemo upandikizaji wa uroto na kuanza kwa uchunguzi wa watoto wachanga.

Amesema, katika kongamano hilo wamewasilisha utafiti uliofanyika kuhusu ubadilishaji wa vinasaba vyenye selimundu kwa watoto wachanga ili kukabiliana na ugonjwa huo.

“Utafiti huu unalenga wale watoto watakaozaliwa na vinasaba vya selimundu wataondolewa vinasaba hivyo na kuwekewa vinasaba visivyo na ugonjwa kwenye damu zao, hii itasaidia kuondoa kabisa ugonjwa huu,” amesema  Prof. Kamuhabwa.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button