Watoto 6 wenye jinsia tata wafanyiwa upasuaji Muhimbili

DAR ES SALAAM; Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imewafanyia upasuaji wa mfumo wa mkojo na haja kubwa watoto 31 na kati ya hao sita walizaliwa na jinsia tata, ambapo upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa MNH kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Ireland na mwingine kutoka Bahrain.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema ni muhimu kwa wazazi kujifungulia kwenye vituo vya afya, ili watoto wakizaliwa waweze kufanyiwa uchunguzi wa kina na kugundulika mapema, ili waweze kupata matibabu mapema.

“Mtoto akigundulika mapema atafanyiwa upasuaji na kurudi katika hali yake
kama inavyotakiwa na mtoto huyo atakapokuwa ataweza kuchangamana na
watoto wengine hata akienda shule atasoma kwa uhuru na kutimiza ndoto zake, ”amesema Prof. Janabi.

Ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwanyooshea watoto vidole pale wanapoona kuwa wanafanya tabia ambazo si za kawaida, badala yake wawapeleke hospitali ili wafanyiwe uchunguzi na kupatiwa msaada.

Akizungumzia umuhimu wa kufanya uchunguzi mapema, daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa watoto MNH, Dk Petronilla Ngila amesema mtoto anaweza akazaliwa akaonekana kuwa na maumbile ya kiume, ila ndani unakuta anazo homoni za kike na endapo akikuzwa kama mtoto wa kiume akifikia kipindi cha balehe ataanza kuingia kwenye siku zake kama mtoto wa kike.

“Mtoto anayezaliwa akiwa na maumbile ya kiume akichelewa kufika hospitali itakuwa ngumu kumrudisha katika hali yake ya kike, kwakuwa jamii itaanza kumshangaa na wengi wanaokuja katika hatua hizi wanaogopa kurudi katika hali zao, hivyo tunawafanyia upasuaji kuondoa yale maumbile ya kike, ili aendelee kubaki kuwa kama mwanaume ingawa hatokuwa na uwezo wa kupata mtoto,”amesema Dk Petronila.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo daktari bingwa bobezi wa upasuaji mfumo wa mkojo na upandikizaji wa figo Dk Gabriel Mtaturu, amefafanua kuwa kati ya watoto 5,000 wanaozaliwa mmoja ana jinsia tata na kati ya watoto 300 mmoja anazaliwa akiwa na jinsia zilizoungana.

Amesema watoto waliofanyiwa upasuaji walikuwa katika makundi manne ambapo baadhi walikuwa na jinsia tata,wengine walikuwa na maumbile ya kike ila ndani walikuwa na maumbile ya kiume, mmoja alikuwa na sehemu mbili za kutolea haja ndogo na mwingine alikuwa wa kike ila hana sehemu za siri, hivyo walimfanyia upasuaji rekebishi na kumtengenezea maumbile ya kike.

#MwangwiwaUkarimu #echoesofkindness
#HabarileoUPDATES

Habari Zifananazo

Back to top button