Watoto 800 hugundulika na saratani kila mwaka

Watoto 800 hugundulika na saratani kila mwaka Tanzania

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu  amesema kila mwaka takriban watoto 800, hugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani nchini Tanzania, hivyo kuchangia ongezeko la vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Waziri Ummy amesema hayo leo, katika kikao  na taasisi ya Global Hope, iliyoko Texas nchini Marekani, katika mkutano wa pembezoni baada ya Mkutano Mkuu wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), unaoendelea New York, nchini Marekani.

“Kila mwaka takriban watoto 800 hugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani nchini Tanzania, lakini kama serikali tumeendelea kuboresha matibabu ya saratani kwa watoto, ili kuokoa maisha yao,” amesema Waziri Ummy.

Advertisement

Amesema kuwa, inakadiriwa watoto wenye saratani wanaoendelea kuishi zaidi ya miaka miwili kuanzia kugundulika ni kati ya asilimia 20 hadi hadi 40, huku katika nchi zilizoendelea ni zaidi ya asilimia 80.

Amesema hali hiyo ni kutokana na  kuchelewa kufanya uchunguzi, kuasi matibabu,  gharama za usafiri na malazi,  uchache wa vituo vinavyofanya uchunguzi na uhaba wa watumishi wenye ujuzi.

Waziri Ummy amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Global Hope, Dk. David Poplack, kwa msaada wanaoipatia serikali ya Tanzania kwa  kufadhili programu ya kuwajengea uwezo watumishi 10, hususan katika fani za ubingwa bobezi wa matibabu ya saratani na magonjwa ya damu  na kutoa vifaa vya uchunguzi katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia ameiomba taasisi hiyo kuongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa ufadhili wa mafunzo ya utoaji huduma za saratani kwa kada za uuguzi, madaktari, wafamasia na wataalamu wa maabara.

Pia amemuomba kujengea uwezo hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya katika kutoa huduma hizo, kwa kujenga na kuipatia vifaa vya kisasa vya huduma za saratani.

Kwa upanda wake Dk Polack ameeleza kuwa, taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya kuimarisha huduma za saratani nchini.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *