UBALOZI wa Ireland nchini, umeunga mkono programu maalumu ya kutoa elimu kwa
watoto juu ya usafi wa mazingira iliyoanzishwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya
‘Success Hand Initiative’ yenye lengo la kuwapa ufahamu watoto juu ya mazingira.
Hatua hiyo imekuja zikiwa zimebaki siku 15 kuelekea siku ya usafi duniani ambapo
shirika hilo leo Septembea 2, 2022 limezindua programu ya kutoa elimu kwa watoto
juu ya usafi wa mazingira.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Programu
hiyo, Asmini Gombo amesema Septemba 17, 2020 itakuwa siku ya usafi duniani,
lakini pia watatembelea shule kwa lengo la kutoa elimu na kufunga programu hiyo.
“Lengo letu watoto wasome vitabu, wajifunze ujasirimali wajitegemee kifedha pia,
nadhani baada ta hapo watoto watakuwa wamepata mwanga mzuri juu ya mazingira
yaliyowazunguka,” amesema Gombo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mary Nsia ameushukuru Ubalozi wa Ireland kwa
kuwaunga mkono katika uendeshaji wa programu hiyo na kwamba wataendelea
kushirikiana na wadau katika kutekeleza malengo ya shirika hilo.
“Bila kusahau kuwa tunapewa nguvu na ubalozi wa Ireland ni hatua nzuri sana kwa
shirika lakini pia tunawashukuru sana kwa kutuunga mkono,” amesema Nsia.
Aidha balozi wa uhifadhi wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais , Benard Paul
amelipongeza shirika hilo kwa kuanzisha programu hiyo na kwamba atakuwa bega
kwa bega na taasisi hiyo katika kutoa elimu kwa watoto.
Naye balozi wa uhifadhi wa mazingira kutoka katika ofisi hiyo, Mwasiti Almasi
ametoa wito kwa shirika hilo juu ya kuendelea kutoa elimu kwa watoto ili
kuwawezesha katika kulinda mazingira ya kizazi cha baadaye.