Watoto milioni mbili kuchanjwa kuepuka Covid-19

Watoto milioni mbili kuchanjwa kuepuka Covid-19

SERIKALI imeanza kutoa chanjo dhidi ya Covid-19 kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano na 11 na inatarajiwa kuwa zaidi ya watoto milioni mbili watanufaika na mpango huo nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Huduma za Afya ya Msingi, Dk Tharcisse Mpunga, muundo maalumu unasimamiwa katika dozi mbili kwa muda wa wiki nne hadi nane kati ya dozi zote mbili za chanjo aina ya Pfizer iliyoidhinishwa na mashirika tofauti ya udhibiti ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda.

Utoaji wa chanjo hiyo kwa watoto wa umri kati ya miaka 5 na 11 ulianza hapa nchini Septemba 20, mwaka huu ukilenga kupunguza mzunguko wa virusi katika jamii.

Advertisement

“Idadi ya watoto walioambukizwa au kufariki kwa Covid-19 bado ni ndogo. Tunawahimiza wazazi walio na watoto kati ya umri wa miaka 5-11 kusaini hati ya ridhaa ili watoto wapate chanjo,” alisema Mpunga.

Takwimu kutoka Kituo cha Afya cha Rwanda (RBC) zinaonesha kuwa, hadi Septemba 18, mwaka huu kati ya wagonjwa 132,488 wa Covid-19 walioripotiwa nchini hapa, watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 11 walikuwa 4,358 sawa na asilimia 3.3 ya wagonjwa wote.

Wakati huo huo; hadi Septemba 18, kulikuwa na watu 9,174,616 nchini Rwanda waliokuwa wamepata dozi ya kwanza ya chanjo hiyo, kati ya hao, walikuwa 8,945,720 waliopata chanjo ya pili huku 316,615 walipata nyongeza.