Watoto wajitokeza utalii Karibu Kusini
IDADI kubwa ya watoto imejitokeza kushuhudia Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yanayoshirikisha mikoa 10 ya Kusini hatua iliyopongezwa na wadau wa utalii waliosema wamepata fursa ya kujifunza.
Diwani wa kata ya Mkimbizi, Elliud Mvella ni mmoja wa wadau aliyeonesha kufurahishwa kuona kuna idadi kubwa ya watoto katika maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka mjini Iringa akisema:
“Sio jambo la kubeza kuona kuna idadi kubwa ya watoto katika maonesho haya kuliko hata watu wazima. Hii ni fursa kwa watoto hawa kujifunza kuhusu tamaduni, lugha, na historia ya mikoa inayoshiriki maeneo wanayotembelea, na vivutio na bidhaa za utalii zinazotangazwa.
Mvella alisema kwa kupitia maonesho hayo watoto wanaweza kujifunza umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kuwachochea kuwa wabunifu, kuwafundisha uwajibikaji na maadili mema na kwa kupitia safari za utalii ni fursa nzuri kwa familia kuungana na kufanya mambo pamoja.
Pamoja na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego kwa maandalizi mazuri ya maonesho hayo Mvella alisikitishwa na ushiriki mdogo wa viongozi wakuu wa baadhi mikoa akisema kutoonekana kwao kunazorotesha juhudi za pamoja za kuyafanya yawe bora zaidi na kuvutia wadau wengi zaidi.
“Kama viongozi wa mikoa na halmashauri za mikoa yote ya kusini wanashiriki vizuri maonesho ya wakulima ya nanenane yanayofanyika kila mwaka mkoani Mbeya, kwanini ushiriki wao katika maonesho ha ya utalii yanayofanyikia hapa Iringa ni wa kusuasua?” alisema.
Maonesho hayo yaliyoshirikisha waoneshaji 135 katika viwanja vya Kihesa Kilolo mjini Iringa kuanzia Septemba 23 na kufungwa leo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe yalikwenda sambamba na kongamano kubwa la uwekezaji lililowavuta wawekezaji zaidi ya 170 pamoja na safari za kutembelea vivutio mbalimbali vya wilayani Iringa.
Akifunga maonesho hayo, Kigahe alipongeza juhudi za mikoa ya kusini katika kukuza utalii na shughuli zake akisema serikali inawaunga mkono na itahakikisha jitihada hizo zinafanikiwa.
Aliziagiza halmashauri za mikoa hiyo kuweka mazingira wezeshi kwa kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo ya utalii.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema muelekeo wa mikoa ya kusini unalenga kuimarisha sekta ya utalii ili mchango wake katika ukuaji wa uchumi na pato la mtu mmoja mmoja uiwiane na wingi wa vivutio vilivyoko katika mikoa hiyo.
Aidha alisema mikoa hiyo ya kusini imejipanga kikamilifu kuhakikisha awamu ya pili ya filamu ya royal tour itakayogusa vivutio vilivyoko katika mikoa ya kusini inafanikiwa.
“The royal tour awamu ya pili inakuja na inaelekezwa kusini. Tunamkaribisha Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kusini, tuna vivutio vingi na kwa kupitia juhudi tunazoendelea kuzifanya za kuvitangaza vitakuwa chanzo kizuri kwa ukuaji wa uchumi,” alisema.