ARUSHA: Idadi ya watoto waliokufa maji kutokana na gari walilikuwa wamepanda kusombwa na maji imefikia watano baada ya miili mingine kupatikana kutokana na juhudi za uokozi zinazoendelea.
Taarifa kutoka katika Kituo cha Afya cha Murriet ambapo miili imehifadhiwa zimesema hadi sasa watoto waliopatikana kuwa wamekufa ni watano. Hata hivyo watoto watatu; Glory Daniel (8), Preygod Daniel (10), Rose Immanuel (10) na Mwalimu Annastazia Immanuel (27) wapo hospitalini kwa ajili ya matibabu kutokana na ajali hiyo.
Awali iliripotiwa kuwa mtoto mmoja amefariki na wengine saba kutojulika walipo baada ya gari la Shule yao ya Ghati Memorial School kusombwa na maji alfajiri ya leo wakati wakijaribu kuvuka korongo la Engosengiu kata ya Sinoni mkoani Arusha.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alifika katika eneo la ajali na kulaumu uzembe wa dereva huyo uliosababisha kifo cha watoto hao na wengine kutojulikana walipo.
Katika mazungumzo na wanahabari katika kituo cha afya cha Murriet, watoto walionusurika ajali hiyo wamemlaumu dereva kuwa alipuuza tahadhari aliyopewa na matroni, Mwalimu Annastazia.
Mtoto mwenye umri wa miaka 8, Glory Daniel amesema “Uncle Lukuman (Lukuman Daniel – dereva) amesababisha yote haya.”