Watoto wawageuka mama zao ugomvi wa ardhi
MANYARA; Mbulu. MIGOGORO ya ardhi na mali imeshika kasi Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, huku akina mama wakikabiliwa na mashambulizi kutoka kwa watoto wao wenyewe wanaojaribu kuwanyang’anya ardhi.
Changamoto hiyo imeelezwa kutokea baada ya kifo cha mume wa mwanamke husika, ambapo watoto hulazimisha kuingia katika umiliki wa mali na kuwasukuma mama zao nje ya ardhi.
“Hii ndiyo changamoto inayokabili jamii nyingi za Mbulu na maeneo mengine ya vijijini katika Mkoa wa Manyara,” amesema Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mji wa Mbulu, Tomic Simbeye ambaye anaongoza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Kwa mujibu wa ofisa huyo akiwa katika kampeni hiyo ya kutembelea jamii, amesema tatizo hutokea kwa sababu wanaume wengi hawana utamaduni wa kuandika wosia, kwa hiyo wanapofariki dunia, migogoro huibuka katika familia zao, ambapo watoto hupigana na mama zao ama wenyewe ili kurithi mali.
“Tukiwa katika jamii hii tuligundua kwamba watoto wanapigana wao na mama zao wenyewe wakigombea ardhi na imechangiwa na kukosekana kwa elimu ya kutosha ya masuala ya ardhi, ambapo sasa kampeni hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ndio itasaidia jamii kutatua masuala mbalimbali yanayowakabili,” amesema Simbeye.
Ofisa huyo ameleza kuwa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’, imeweza kuzifikia kata 17 za Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kufanya mikutano ya hadhara ya zaidi ya watu 8000 katika eneo hilo.
“Tulilenga kufikia angalau watu 1000 kwa kila kata, lakini tulifanikiwa kufikia 8000 kwa jumla,” amesema, na kuongeza kuwa mara nyingi wakazi wa eneo hilo walikuwa na shughuli nyingi za kila siku, hivyo kushindwa kuhudhuria mikutano lakini wamepanga kurudi tena baadaye kwa ajili ya kutoa elimu zaidi kwa jamii.
Masuala mengine yaliyogunduliwa wakati wa kampeni hiyo ni pamoja na matukio ya ukatili wa kijinsia, wasichana kuachwa baada ya kupata mimba, watu kushindwa kupima ardhi, ndugu kupigania mirathi.
Amefafanua kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni ya miaka mitatu ya kutafuta ukweli na kutatua matatizo mbalimbali katika jamii ikilenga kufikia mikoa, wilaya na kata zote Tanzania bara na visiwani.
Baada ya Dodoma, Manyara, Sinyanga na Simiyu kampeni sasa imehamia Mkoa wa Singida kuanzia mwezi huu wa Novemba 2023 huku Ujumbe husika ni kushughulikia ukatili wa kijinsia, migogoro ya kijinsia, ndoa na mirathi.