Watu 100 wafa maji wakitoka harusini

NIGERIA: ZAIDI ya watu 100 wakiwemo watoto  wamekufa maji katia ajali ya boti iliyopinduka kaskazini mwa Nigeria ikiwa na familia zilizokuwa zikirejea makwao kutoka kwenye hafla ya harusi, maafisa wa polisi wamethibitisha.

Wakaazi na polisi bado walikuwa wakitafuta makumi ya watu waliokuwa kwenye boti hiyo iliyozama mapema Jumatatu kwenye Mto Niger katika wilaya ya Pategi jimbo la Kwara, ambalo ni kilomita 160 kutoka Ilorin, mji mkuu wa jimbo hilo, Msemaji wa Polisi, Okasanmi Ajayi amesema Jumanne.

Alisema hadi sasa watu 100 wameokolewa. Hii sio mara ya kwanza kwa ajali kama hizi, mwaka jana watu 76 walikufa maji katika boti iliyokuwa imebeba watu zaidi ya 100 kupata hitilafu ya injini na kushindwa kuhimili mawimbi ya maji.

Advertisement

Wengi wa waliokufa maji walikuwa jamaa kutoka vijiji kadhaa waliohudhuria harusi pamoja na kushiriki karamu hadi usiku, kulingana na Abdul Gana Lukpada, chifu wa eneo hilo. Walifika kwenye hafla hiyo kwa pikipiki lakini walilazimika kuondoka kwa boti iliyotengenezwa kienyeji baada ya mvua kunyesha na kuharibu barabara, alisema.

“Boti ilikuwa imejaa kupita kiasi na karibu watu 300 walikuwa ndani yake. Walipokuwa wanakuja, boti iligonga gogo ndani ya maji na kugawanyika vipande viwili,” alisema Lukpada.

Harusi ilifanyika katika kijiji cha Egboti katika jimbo jirani la Niger, alisema Usman Ibrahim, mkazi wa eneo hilo. Kwa sababu ajali hiyo ilitokea saa 3 asubuhi, ilikuwa saa chache kabla ya watu wengi kujua kilichotokea, alisema.

Wakati abiria hao wakizama, wanakijiji waliokuwa karibu walikimbilia eneo la tukio na kufanikiwa kuwaokoa takriban watu 50, Lukpada alisema, akielezea juhudi za mapema za kuwaokoa abiria hao kuwa zilikuwa taratibu na “ngumu sana”.

Taarifa za kina kuhusu ajali hiyo iliyotokea katika jimbo la Kwara bado haijatolewa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *