JESHI la Polisi mkoa wa Morogoro, linawashikilia watu 101 kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali, yakiwemo wizi wa simu na mikoba ya wanawake, wakitumia pikipiki na bajaji ( Vishandu), uvunjaji, upokeaji na ununuzi wa mali za wizi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fortunatus Musilimu, amesema hayo leo kwa waandishi wa habari, kuhusu operesheni kali inayoendelea ya kupambana na uhalifu, ambayo ilianza Septemba 12, mwaka huu .
Musilimu amesema katika oparesheni hiyo watu 101 walikamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali, ikiwemo kukamatwa pikipiki 10 za aina mbalimbali zisizo na namba za usajili, zinazosadikika zikitumiwa na baadhi yao kufanikisha uhalifu huo.
Amesema watuhumiwa walikamatwa kutoka maeneo ya Kihonda, Chamwino, Msamvu, Nanenane, Kichangani, Tungi, Mwembesongo, Mafisa na Mbuyuni ndani ya Manispaa ya Morogoro.
Musilimu amesema kati ya watuhumiwa hao, 91 ni wanaokujihusisha na uhalifu wa kutumia pikipiki (Vishandu).
Ametaja vitu vingine ambavyo walikamatwa navyo , ni simu janja 10 za aina mbalimbali na televisheni za kisasa.
Pia amesema katika operesheni hiyo walikamata gari aina ya Land Cruiser, iliyobandikwa namba bandia N 5978 S na Mercedes benz yenye namba za usajili T .962 BYH, ikiwa ndani ya Fuso lenye namba za usajili T.567 BRR.