WATU 15 wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia shambulizi katika kanisa katoliki Kaskazini Mashariki mwa Burkina Faso jana.
Tukio hilo limetokea kijiji cha Essakane katika jimbo la Oudalan karibu na mpaka na Mali.
Ofisa mmoja wa kanisa hilo alidokeza kwamba watu hao wenye silaha wanashukiwa kuwa kundi maalum la wanamgambo wenye itikadi za kidini.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa mamlaka katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Ouagadougou.
Taarifa ya mkuu wa Dayosisi ya eneo hilo, Abate Jean-Pierre Sawadogo, ilisema watu 12 waliuawa papo hapo, huku wengine watatu wakifia hospitalini.
“Katika hali hii mbaya, tunakualika kuwaombea waliokufa kwa imani, uponyaji wa majeruhi, na uimarishaji wa mioyo ya huzuni,” inasomeka taarifa hiyo.