Watu 200 kunufaika na Voda Bima Iringa

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa imepokea msaada wa kadi za Bima ya Afya kwa mama na watoto 200 kutoka kwa kampuni ya tekenolojia ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia kampeni yake ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha.’

Baadhi ya wanawake na watoto wenye sifa za kupata kadi hizo zitakazowawezesha kupata huduma za matibabu bure kwa mwaka mzima katika hospitali yoyote nchini, wamekabidhiwa zawadi hiyo ya upendo toka kwa kampuni hiyo katika tukio lililofanyika hospitalini hapo leo.

“Tunashukuru kampuni hii kwa kuguswa na changamoto za wanawake na watoto na kuamua kutoa bima za mwaka mzima kwa walengwa 200 katika mkoa wetu,” alisema Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Scolastica Malangalila.

Dk Malangalila alisema tayari walengwa 31 wamenufaika na msaada wa bima za kampuni hiyo huku juhudi za hospitali hiyo kuwapata wengine wenye vigezo zikiendelea.

Dk Malangalila aliisifu kampuni hiyo kwa kuona jambo hilo linaweza kuwafaa wateja wa hospitali hiyo hususani wanawake na watoto ambao mahitaji yao ya huduma za afya ni makubwa.

“Tungetamani kuona akina mama wote wanaokuja hospitalini kujifungua wanakuwa na bima za afya.

Tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ambaye hivikaribuni amesaini muswada wa Bima ya Afya kwa wote kuwa sheria kamili itakayowezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa watanzania pasipo na kikwazo cha uchumi,” alisema.

Akikabidhi kadi hizo, Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Vodacom Tanzania PLC, Abednego Mhagama alisema wametoa bima hizo kama sehemu ya mpango wa kampuni yao ya kurudisha kile wanachopata kwa wateja wao na kwa kutambua kwamba watanzania wengi wanaelemewa na gharama za matibabu na hawana uwezo wa kuzimudu.

Alisema matibabu ya afya kwa akina mama siku zote yana nafasi muhimu kwa Vodacom na kwa kuzingatia kuwa huu ni msimu wa sikukuu ambao hujumuisha jamii na kujitolea, wameona ni vyema kutumia huduma yao bunifu ya kidigitali ya bima ijulikanayo kama Vodabima kusambaza shangwe na kugusa maisha ya akina mama na watoto wao.

“Tumetoa bima 200 kwa hospitali hii, zoezi la kusajili walengwa linaendelea kwasababu bado halijakamilika. Usajili unafanywa kwa akinamama waliojifungua msimu wa sikukuu kuanzia Desemba 9 mwaka jana,” alisema na kuongeza kwamba kundi hilo ndilo linalokumbwa na maradhi ya hapa na pale katika hatua za awali hivyo kuwa mzigo kwa watu wengi kumudu gharama za matibabu.

“Kwa msaada huu wa bima kubwa za afya kwa kipindi cha mwaka mmoja, hakika tutakuwa tumewasaidia walengwa hao 200 na kuwapa fursa ya kujipanga kwa siku za usoni,” alisema.

Mmoja wa mama aliyepokea bima ya afya pamoja na mtoto wake, Grace John alisema; “nimepokea msaada huu kwa furaha na najiona mwenye bahati kupatiwa bima ya afya ya bure kwa mwaka mzima mimi pamoja na mtoto wangu. Nawashukuru Vodacom na wateja wao kwa kutukumbuka wanawake tusio na uwezo.”

Kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ ya Vodacom Tanzania ilizinduliwa Novemba 2023 ikilenga hadi Januari mwaka 2024 kuwafikia akina mama na watoto 2000 nchini kote.

Habari Zifananazo

Back to top button