Watu 36 waliwa na mamba Buchosa

DODOMA; MBUNGE wa Buchosa, Eric Shigongo amesema bungeni kuwa, watu 36 wameliwa na mamba kwa nyakati tofauti jimboni kwake.

Kutokana na hali hiyo amemba Muongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 54, akiomba kuahirishwa shughuli za Bunge, ili liweze kujadili suala hilo kama jambo la dharura, kwani wananchi wake wanaliwa na mamba.

Amesema ingawa kuna sheria ya kimataifa ya kutaka mamba alindwe, lakini haki ya kuishi ya mwanadamu lazima izingatiwe pia.

Akitoa maelezo yake Mbunge Shigongo, amedai kuwa tukio la karibuni mtu kuliwa na mamba lilitokea Aprili 14 mwaka huu, ambapo mama mmoja aliliwa na mamba na kufanya kuwe na ongezeko kubwa la yatima jimboni kwake.

Amesema ingawa idadi hiyo ya watu kuliwa na mamba ni katika kipindi cha miaka mitatu, lakini idadi kubwa zaidi wameliwa siku za karibuni.

“Binadamu lazima aishi kwanza kabla mamba hajaishi… Naanza kuona kwamba mamba anaweza kuwa na thamani kuliko binadamu wa Buchosa, kwa misingi hiyo Mheshimiwa Spika nilikuwa naomba sana tutafute namna yoyote ya kujadili kama wabunge ili tuweze kuishauri Wizara ya Maliasili na Utalii, tutafanya nini ili kuweza kuokoa maisha ya watu,” amesema.

Akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema Bunge linajali maisha ya watu hata angekuwa mtu mmoja.

“Hata kama angekuwa amefariki mtu mmoja ni kazi yetu kama Bunge kuishauri Serikali juu ya hatua za kuchukua,” amesema na kuongeza kuwa kanuni ya 55 inaweka masharti juu ya jambo gani linafaa kujadiliwa kama la dharura.

Amesema kwa vile leo Wizara ya Maliasili na Utalii inawasilisha bajeti yake na itajadiliwa hadi Jumatatu, ni vyema Mbunge huyo na wengine wakatumia fursa hiyo kuchangia mawazo yao na kuishauri serikali itayachukua ili kufanyia kazi.

“Hatutaweza kujadili kama jambo la dharura, lakini serikali imesikia hoja za Mbunge wa Buchosa,” amesema Spika.

Habari Zifananazo

Back to top button