Watu 43 wafanyiwa upasuaji Bombo

KAMBI maalum ya Upasuaji wa Kurekebisha Viungo iliyoanza Julai 17, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga ‘Bombo’ imefanikiwa kuwafanyia upasuaji watu 43 kati ya 86 hadi kufikia leo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo leo Julai 24, 2023 na kusema kuwa upasuaji huo unaofanywa na madaktari bingwa kutoka Ujerumani na Tanzania sio kama ule wa ‘wadada’ wa kisasa bali huu ni upasuaji wa Viungo ili kuvirejesha katika utendaji wake wa kawaida.

“Nimeshuhudia wagonjwa ambao wamekatwa miguu yote miwili (baada ya kupata ajali au maambukizi yaliyopelekea kukatwa miguu) sasa wanatembea kwa miguu bila fimbo au msaada wowote baada ya kuwekewa ‘miguu’. Hakika ni jambo la kutia faraja na kuendelezwa,” amesema Waziri.

Advertisement

Aidha, alimshukuru Professor Juergen Dolderer na Taasisi yake ya Interplast German na University Medical Centre, Bayreuth German kwa kuichagua hospitali ya Bombo kuwa mshirika wa kutoa huduma hizo nchini ikiwemo kuwajengea uwezo wataalam wa kitanzania kufanya upasuaji wa kurekebisha viungo.

Mahusiano ya Tanga na Ujerumani ni ya kihistoria. Inasadikika kuwa Bombo ndio hospitali ya kwanza kujengwa na wajerumani ktk ukanda huu wa Afrika Mashariki.

“Nawashukuru mno Interplast kwa kukubali ombi letu la kuifanya hospitali ya Bombo kuwa Kituo cha Umahiri cha Upasuaji wa Viungo (Centre of Excellence on Reconstructive and Cosmetic Surgery) ukanda wa Afrika Mashariki. Tunakamilisha taratibu zote zinazohitajika ili kuyapa nguvu maono haya,” Alisema Waziri Ummy.

5 comments

Comments are closed.