JESHI la Polisi mkoani Mara, linawashikilia watu 44 kwa tuhuma za kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya aina ya bangi kilo 59 na miche 87, pamoja na kukutwa na pombe haramu ya gongo lita 423 na mtambo wa kutengeneza pombe hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase, amesema kukamatwa kwa wahalifu hao ni sehemu ya opereshion maalum ya kupambana na wahalifu mkoani humo.
Kamanda huyo amesema ndani ya mwezi Juni jeshi hilo limepeleka mahakamani kesi 18 kwa watuhumiwa 70, ambapo aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kudhibiti vitendo vya uhalifu.
“Nitoe wito kwa viongozi wa kidini, kimila pamoja na wananchi ambao kwa dhati wamejitoa kuhakikisha mkoa huu unaimarika kwa kudhibiti uhalifu, tuendelee kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha masuala ya uhalifu yanadhibitiwa, ” anasema Morcase.