DODOMA: Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma imefanya upandikizaji wa betri kwenye moyo ‘pacemakers implantation’ kwa watu watano.
Upandikizaji huo umefanyika kwa watu wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na kusababisha mapigo ya moyo kuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kwa mtu wa kawaida ambayo ni 60-100 kwa dakika huku wengi wao huwa ni chini ya 40.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa BMH, Daktari Bingwa wa Moyo, Happiness Kusima, amesema leo Februari 28,2024 kuwa BMH imefikisha upandikizaji kwa watu 18 toka huduma ianzishwe mwaka 2021.
“Jana tumepandikiza watu watatu, leo tumepandikiza watu wawili,” amesema Kusima.
Aidha, amesema upandikizaji huo umefanyika kwenye kambi ya Madaktari Bingwa wa Moyo wa BMH kwa kujengewa uwezo na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya jijini Dar es Salaam.