KAMANDA wa Jeshi la polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa jeshi lao linawashikilia watu saba kwa kosa la kuiba transfoma na nyaya za umeme mali ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wilayani Magu mkoani hapa.
Mutafungwa amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Amebainisha kuwepo kwa vitendo hivyo vya wizi wa vifaa vya umeme na kuuzwa kwa wauza vyuma chakavu.
Mutafungwa amesema Juni 5, 2023 maeneo ya Sagain wilayani Magu zilipatikana taarifa kuwa wahalifu wameshusha Transforma na Jeshi la Polisi lilifika kwa wakati na kumkamata Caroli Clement mwenye umri wa miaka 26 mkulima na mkazi wa Kisesa.
Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa watuhumiwa wengine waliokamatwa katika msako ni Daniel Maige ambae ni mkazi wa Igudija K, John Deogratias ambae mkazi wa Nyamhongolo, Baraka Stanley ambae ni mkazi wa Igoma , Marwa Dismas ambae ni mkazi Kangaye,Wilson Joseph , Ally Tarimo mkazi wa kilimahewa.
Mutafungwa ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya kihalifu ili kuweza kutokomeza vitendo hivyo.