WATU saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria kampuni ya Sheraton lenye namba za usajili T922 ADC iliyotokea katika kijiji cha Mwilima kata ya Kasamwa mkoani Geita.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Amesema, ajali imetokea leo Machi 7, 2023 majira ya saa 10:30 jioni na kueleza chanzo cha ajali ni kupasuka kwa tairi ya mbele ya basi hilo.
Mlay amesema, basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kuelekea Ushirombo mkoani Geita ambapo dereva alipoteza ustahimilivu baada ya tairi ya mbele kupasuka na basi kutumbukia darajani.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita ambapo majeruhi walipelekwa katika kituo cha Afya Kasamwa kwa huduma ya kwanza na kisha hospitali ya rufaa ya mkoa kwa matibabu zaidi.