Watu 804 kulipwa Sh bilioni 1.23 kupisha bomba la mafuta

SERIKALI imetumia Sh bilioni 1.23 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 804 waliosaini mikataba ya fidia na kulipwa ili kupisha mradi wa Bomba la Mafuta ghafi wa Afrika Mashariki kwa Mkoa wa Dodoma.

Wananchi hao ni miongoni mwa wananchi 9,813 kutoka mikoa minane inayopitiwa na mradi huo ambapo mpaka Septemba 21, mwaka huu walikuwa wamesaini mikataba ya fidia na kulipwa Sh bilioni 34.89.

Akizungumza jijini Dodoma, Mratibu wa mradi huo kwa upande wa Tanzania kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Asiadi Mrutu alisema waliolipwa ni kati ya wananchi 810 waliopisha mradi huo kwa Mkoa wa Dodoma, hivyo kufanya waliofikiwa na fidia hizo kwa mikoa minane inayopitiwa na mradi huo kufikia asilimia 99.1.

“Katika wananchi waliopisha eneo la mkuza kwa upande wa Dodoma, wananchi 810 wanatakiwa kulipwa fidia na mpaka sasa hivi wananchi 804 wameshasaini mikataba ya fidia na wamelipwa Sh bilioni 1.23,” alisema.

Mikoa inayopitiwa na mradi huo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Alisema pamoja na wananchi hao kulipwa fidia pia wananchi 293 walikubali kujengewa nyumba kulingana na idadi ya nyumba zilizokuwepo kwenye eneo husika wakati wa tathmini na mpaka sasa nyumba 242 zimekamilika kati ya nyumba 339.

Alisema pia TPDC kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wameweka alama za mipaka kwenye eneo la mkuza lenye kilometa 612.33 kati ya kilometa 1,147 sawa na asilimia 53.39.

Akizungumzia fursa za ajira wakati wa utekelezaji wa mradi huo, Mrutu alisema mpaka Juni 30, mwaka huu Watanzania 3,619 wameajiriwa sawa na asilimia 91 ya wafanyakazi wote.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania lina urefu wa kilometa 1,443 na unatarajia kugharimu Dola za Marekani bilioni 5.088 na litakuwa na uwezo wa kupitisha mapipa 216,000 kwa siku utakapoanza kazi.

Muda wa ujenzi wa mradi huo ni miezi 24 na unatarajia kuanza kutekelezwa Januari mwakani. Kuhusu kazi za awali zinazoendelea, Mrutu alisema kwa sasa kwa upande wa Tanzania ni ujenzi wa makambi ya ujenzi ambapo makambi manne kati ya 12 yamekamilika kwa asilimia 100.

Pia ujenzi wa karakana ya kuandaa mabomba eneo la Sojo mkoani Tabora umefikia asilimia 40 na umetoa ajira kwa Watanzania 426 sawa na asilimia 95 na kampuni 20 za Kitanzania zimetoa huduma zenye thamani ya Sh bilioni 50.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button