Watu 87 Tanzania hufariki kwa TB kila siku

UGONJWA wa Kifua Kikuu au TB ni janga linalouwa kimya kimya ambapo takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania watu 87 hupoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa huo na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 30 duniani zenye maambukizi makubwa ya TB

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma jijini Dar es Salaam, Dokta Mbarouk Seif Khaleif amesema Tanzania kila mwaka watu 137,000 huugua TB na husababisha vifo 32,000, sawa na vifo 87 kila siku kati ya vifo hivyo, 33 ni vya waliokuwa wanaishi na virusi vya ukimwi (WAVIU).

Akizungumza na HabariLeo, Dokta Mbarouk amesema TB ni janga ambalo linaua kimya kimya na hugharimu wastani wa asilimia 7 ya pato la taifa huku Dar es Salaam ikiwa kinara kwa asilimia 17.

Chukua mfano mabasi yanayoenda mkoani, iwe kila siku basi linaanguka watu 87 wanafariki, jamii ingepaza sauti na taadhari nyingi zingechukuliwa ili kuzuia ajali, vivyo  hivyo jamii inapaswa kushiriki kutokomeza ugonjwa huu wa TB ambao ugharimu maisha ya mamia ya watu.” Amesema

Naye Mratibu wa TB wilaya ya TB Mnazi mmoja Dokta Linda Mutasa amesema kumekuwa na dhana potofu kuwa mwenye kifua kikuu lazima awe na ukimwi au amerithi na wengine kwenda mbali na kudai kuwa wamerogwa.

“Ukikohoa wiki mbili mfululizo, kutoka jasho jingi usiku, kupumua kwa shida, uchovu, maumivu ya kifua na homa, ukiona dalili hizo ni vema kuwahi vituo vya afya kwa uchunguzi zaidi.”Amesema

Amesema, serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kuweza kuwafikia na kuwaweka katika matibabu wenye uhitaji wa huduma ya matibabu ya TB hadi kufikia asilimia 64.

“Kila mmoja wetu anawajibu wa kujitolea kwa hali na mali ili kuweza kuwafikia wagonjwa wapatikane ili wapate matibabu na kuyafikia malengo yetu ya kuudhibiti  na kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.”. Amesema

Aidha, amesema kuwa mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajagundulika na kuwekwa katika matibabu ana uwezo wa kuambukiza watu kati ya 10 mpaka 15 kwa mwaka.

Amesema katika kuendeleza juhudi za kudhibiti ugonjwa huo Serikali imeboresha huduma za uchunguzi na uuguzi kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa za  mashine za Gene Xpert 50, Mashine za ECG 179 ambazo utumika kutambua vimelea vya TB kwa haraka na uhakika.

Hata hivyo Mutasa amesema Tanzania ipo katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko wa mfumo wa hewa ambayo mengine yanashabihiana na kifua kikuu pamoja na UVIKO-19.

Habari Zifananazo

Back to top button