Watu mil 21 wahesabiwa siku mbili

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema Watanzania milioni 21 wamehesabiwa katika siku mbili za kwanza za sensa ya watu na makazi, yaani Agosti 23 na 24 mwaka huu.

Dk Chuwa alilieleza HabariLEO Alhamis kwa simu kuwa katika siku ya kwanza walihesabiwa watu milioni 10.26 na Agosti 24 zaidi ya watu milioni 10.

Alisema alitoa takwimu hizo za siku mbili kuwaonesha Watanzania kwamba kazi hiyo itakayofanywa kwa siku saba inaendelea vizuri lakini mwenye mamlaka ya kutoa takwimu za mwisho ni Rais wa nchi hivyo hataendelea kutoa takwimu kuhusu kazi ya sensa inavyoendelea.

“Nilitoa takwimu hizo kuwaonesha Watanzania kwamba zoezi la sensa ya watu na makazi linaendelea vizuri, hakuna changamoto kubwa zilizojitokeza kukwamisha,” alisema Dk Chuwa.

Alisema takwimu ni siri hivyo hairuhusiwi kuzitangaza hadharani kabla ya kuzikamilisha, kujumlisha na kizichakata ili kujua idadi kamili hivyo hataendelea kuzitoa ili pia kuepuka wenye mbinu chafu wanaoweza kuzitumia kwa nia ovu.

Dk Chuwa alisema atakuwa akitoa taarifa za maendeleo ya sensa kwa Baraza la Mawaziri na kwa makatibu wakuu ili waelewe kinachoendelea.

Alisema tangu sensa ya watu na makazi ilipoanza hakuna changamoto kubwa zilizojitokeza kukwamisha kazi hiyo na wananchi wanaendelea kutoa taarifa zao kwa makarani.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button