Watu mil 7 waishi na magonjwa ya akili

Watu mil 7 waishi na magonjwa ya akili

TANZANIA inakadiriwa kuwa na takribani watu milioni saba wanaoishi na magonjwa ya akili.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwenye ufunguzi wa semina kwa wahariri wa vyombo vya habari katika kuadhimisha Wiki ya Afya ya Akili mkoani Dar es Salaam.

Alisema takwimu za duniani zinaonesha kuwa katika mwaka 2021 jumla ya watu walioathirika na aina mbalimbali za magonjwa ya akili duniani ni takribani milioni 970.

Advertisement

“Magonjwa hayo yanahusisha sonona, wasiwasi, kizofrenia na magonjwa ya akili kwa watoto na vijana. Kati yao watu milioni 301 wanasumbuliwa na ugonjwa wa akili aina ya wasiwasi na milioni 280 aina ya sonona tu. Wanawake huwa wanaathirika zaidi kuliko wanaume kwa asilimia 52.4,” alisema Ummy.

Akizungumzia semina hiyo ya wahariri, Ummy alisema wataalamu wamejipanga vyema kuhakikisha lengo la semina hiyo linatimia na anatarajia wahariri hao watatumia muda huo vizuri kujifunza ili kuongeza hamasa zaidi katika kazi za uandishi wa habari katika eneo la afya ya akili.

“Kama mnavyojua hii ni Wiki ya Afya ya Akili Duniani, ambapo tunaiadhimisha kitaifa hapa jijini Dar es Salaam. Kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari, tumeandaa hii semina ili kuongeza uelewa wa pamoja na kuwajengea uwezo juu ya afya ya akili,” alisema.

Katika semina hiyo iliwasilishwa mada kuhusu magonjwa ya afya ya akili iliyoandaliwa na Msaikolojia wa tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Idara ya Afya na magonjwa ya akili, Isaac Lema, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) na Daktari kutoka Hospitali ya Mirembe, Erasmus Mndeme.

Katika wasilisho lao, ilielezwa mtu mzima mmoja kati ya wanne anapitia ugumu wa afya ya akili. Vilevile mtu mzima mmoja kati ya watano mahali pa kazi anapitia matatizo ya afya ya akili.

Asilimia 10 ya wafanyakazi wanatumia muda wa kazi kwa ajili ya sonona na wastani wa siku 36 za kazi hupotea kutokana na sonona kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2017.

Aidha, ilitaja sababu za tatizo la afya ya akili kuwa ni mtu kushindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, vinasaba, vilevi, magonjwa ya mwili  kama vile Ukimwi na malaria kali, msongo wa kiwango cha juu, shinikizo la makundi rika na matukio yenye tishio la maisha kama vile majanga, ukatili, unyanyasaji na migogoro.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO ya mwaka 2019, kila baada ya sekunde 40 kuna mtu anajiua kwa sababu mbalimbali. Juzi shirika hilo limesema Afrika ina kiwango kikubwa zaidi cha watu wanaojiua duniani.

1 comments

Comments are closed.