Watu milioni 15 wapata chanjo Covid-19

Ofisa Programu wa Uelimishaji Jamii kutoka Wizara ya Afya, Juliana Mshama

WATANZANIA milioni 15.92 tayari wamepata chanjo kamili dhidi ya Covid- 19 huku takwimu zikionesha kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu wasiokamilisha dozi.

Ofisa Programu wa Uelimishaji Jamii kutoka Wizara ya Afya, Juliana Mshama alisema kuwa mpaka sasa waliopata chanjo kamili ni asilimia 51.92 kati ya watu 30,740,643 wanaotarajiwa kupatiwa chanjo hiyo. Alisema lengo la serikali ni kutoa chanjo kwa angalau asilimia 70 ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ifikapo Desemba, mwaka huu.

“Waliopata chanjo kamili Tanzania ni 15,960,643 sawa na asilimia 51.92 kati ya 30,740,928 waliokusudiwa kwa kuzingatia wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,” alisema. Alisema wakati Tanzania Bara walengwa ni 15,764,977 (sawa na asilimia 26.49) kati ya Watanzania 59,517,754, ambayo ni sawa na asilimia 52 kati ya watu 30,053,428 (wenye miaka 18+) waliokusudiwa kwa Tanzania Bara.

Advertisement

Katika kampeni yake serikali imelenga kuchanja Watanzania 59,744 wenye umri wa miaka 18+ kwa siku. Akizungumzia ukamilishaji wa dozi alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha watu l,775,398 waliotakiwa kukamilisha dozi ya pili ya Sinopharm na Pfizer Julai 31, mwaka huu hawakukamilisha. Pia takwimu za Wizara hiyo zinaonesha watu 872,821 waliotakiwa kurudi kukamilisha dozi hizo Agosti 14, hawakufanya hivyo.

Pia alisema watu 416,869 kati ya 1,719,296 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer hawakurudi. Aidha, watu 455,952 kati ya 2,728,575 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm hawakurudi. “Watu 449,416 kati ya 1,712,107 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer hawakurudi. Watu 325,982 kati ya 2,439,250 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm hawakurudi,” alisema.

Pia alisema takwimu za kidunia, kwa wiki iliyopita idadi ya wagonjwa wapya imeongezeka kwa kanda ya Pacific Magharibi kwa asilimia 52, Mediterranea Mashariki asilimia 45 na Kusini Mashariki Asia kwa asilimia 13. Alisema kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Julai 27, mwaka huu hadi kufikia Julai 25, 2022 jumla ya dozi bilioni 12.24 za chanjo ya Covid-19 zilitolewa duniani.

Utoaji wa chanjo dhidi ya Covid-19 hapa nchini ulizinduliwa Julai 28, mwaka 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo chanjo aina ya Pfizer, Moderna, Sinopharm, Sinovac na Jansen ziliidhinishwa kutumika nchini.

Hivi karibuni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2 hadi 29 jumla ya watu 543 walithibitika kuwa na maambukizi ya Covid-19; ukilinganisha na wagonjwa 352 kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita kuanzia Juni 4 hadi Julai mosi mwaka huu. Alisema kuwa hilo ni ongezeko la asilimia 54.3, katika kipindi hicho hakuna kifo kilichotokea kutokana na Covid-19.

Alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Julai watu waliothibitika kuwa na ugonjwa huo walitoka mikoa ya Dar es Salaam (356), Mwanza (41), Mbeya (24), Shinyanga (20), Katavi (19), Arusha (16), Lindi (13), Kilimanjaro (12), Mtwara (12), Mara (7), Simiyu (5), Tabora (2), Kagera (2), Morogoro (2), Iringa (1) na Dodoma (1).

Alisema kuwa jumla ya wagonjwa 10 waliothibitika kuwa na Covid-19 walilazwa na wote walikuwa hawajapata chanjo, hali inayoashiria kuwa maambukizi yameongezeka katika jamii ikilinganishwa na mwezi Juni. Dk Sichalwe alisema kuwa Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo ili kuwawezesha wananchi kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Alisema kuanzia Julai 2 hadi 29 mwaka huu jumla ya wananchi waliopata dozi kamili ya chanjo ya Covid-19 ni 4,223,670 hilo likiwa ni ongezeko la watu 1,182,519 likilinganishwa na kiwango cha uchanjaji mwezi mmoja uliopita Juni 4 hadi Julai mosi ambapo watu 3,041,151 walipata chanjo hiyo.

Alisema Wizara itaendelea kuwahimiza wananchi kupata na kukamilisha dozi za chanjo ya Covid-19 ili kuzuia kupata ugonjwa mkali hata kusababisha kifo pale mtu anapopata maambukizi.