Watu milioni 3 wanusurika kupata mabusha Dar

DAR ES SALAAM: WATU milioni 3.7 wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamenusurika kupata maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa Mabusha na Matende kutokana na kutokuwepo kwa maambukizi mapya katika Manispaa ya Temeke,Jiji la Dar es Salaam na kata 10 za Manispaa ya Kinondoni .

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hatua zilizofikiwa kutokomeza ugonjwa huo nchini Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema bado kata 10 za Manispaa ya Kinondoni zinakumbwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Ummy amesema wanasitisha zoezi la utoaji wa kinga tiba katika maeneno ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo hayana maambukizi mapya huku kata 10 za Kinondoni zikiendelea na matumizi ya dawa kinga hizo.

Advertisement

“Tutaendelea na zoezi la kampeni za umezeshaji wa kingatiba katika kata 10 za Manisapaa ya Kinondoni ambazo Tandale, Kijitonyama, Mwananyamala, Kigogo, Mzimuni, Magomeni  ,Ndugumbi, Hananasif, Kinondoni na Makumbusho ambazo zinamaambukiza bado kwa asilimia 2.3,”amesisitiza Ummy.

Amesema kwa upande wa Dar es Salaam mwezi Machi na Agosti ,2023 na Mwezi Februari 2024 walifanya thamini ya kiwango cha maambukizi na matokeo yalionesha Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni na Manispaa ya Ubungo hazina maambukizi mapya kwa kipindi cha miaka sita baada ya kusitisha umezeshaji kingatiba.