Watu zaidi ya milioni 1 wakimbia Sudan

 

KHARTOUM, Sudan

TAKRIBANI wakimbizi 250,000 wamevuka na kuingia nchi jirani na Sudan tangu Aprili 15, 2023 baada ya mzozo kati ya Jenerali wa Jeshi, Abdel Fattah al-Burhan na Mkuu wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Mohamed Hamdan “Hemedti” Dagalo, kugeuka kuwa mzozo wa silaha.

Advertisement

Watu wengine 843,000 wamekimbia makazi yao ndani, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) lilisema na kufanya jumla ya watu waliokimbia makazi yao katika kipindi cha wiki sita zilizopita kufikia zaidi ya milioni moja.
Wakati mapigano mengi mabaya zaidi yametokea katika mji Mkuu wa Sudan, Khartoum, vita vikali pia vilitokea katika eneo la Magharibi mwa nchi hiyo la Darfur, kati ya jamii za Waarabu na Wamasalit. Ghasia hizo zimewalazinu wakimbizi 60,000 kukimbilia nchi jirani ya Chad.

Mashirika ya misaada yanasema idadi ni kubwa zaidi kwani watu wanaendelea kumiminika kila siku nchini, na maelfu hawajasajiliwa kufikia sasa.

Wakimbizi wengi wako katika makazi yasiyo rasmi mpakani na wako hatarini kutokana na mapigano iwapo hawatasogezwa ndani zaidi nchini kabla ya msimu wa mvua kuanza katika takriban wiki nne.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilianza kuwahamisha takriban watu 1,000 siku ya Jumatatu huku kukiwa na changamoto kubwa ya vifaa na uhaba wa fedha.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *