Watuhumiwa 2,397 wadakwa matukio dawa za kulevya
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imeteketeza kilogramu 11, 766.
88 katika kipindi cha Julai 1, 2022 hadi Septemba 30, 2022.
Hayo yamesemwa na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Gerald Kusaya katika maonesho ya wiki ya vijana mkoani Kagera.
Amesema katika operesheni mbalimbali walizofanya kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwaka wa fedha wa Julai, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 2,397, ambapo kati yao watuhumiwa 29 ni wa dawa aina ya Cocaine, watuhumiwa 179 ni wa Heroine, watuhumiwa 1,934 ni wa bangi na watuhumiwa 244 ni wa mirungi.
Kusaya amesema katika kipindi hicho, wameteketeza kilo 22.
6 za Heroine, gramu 366 za cocaine, kilo 6,680.43 za bangi na kilo 4,397.79 za mirungi.
“Ukiangalia tatizo kubwa linalotukabili kwa sasa ni bangi, tumeweza kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya kwa njia ya ndege, bandari tunajitahidi kudhibiti kwa vikosi vyetu vya doria, Bandari ya Tanga na Mtwara, ila bado kuna changamoto kama mnavyojua bahari ni dude kubwa, ila tunajitahidi kudhibiti zisiingie,” amesema Kusaya.
Akizungumzia maonesho hayo Kusaya amesema, DCEA imeshiriki ili kutoa elimū kwa vijana kuhusu athari za dawa za kulevya.
Maonesho hayo yameanza Oktoba 8 na yatafikia kilele chake Oktoba 15 katika viwanja vya Gymkhana mjini Bukoba.
Amesema ili kudhibiti dawa za kulevya nchini, ushirikiano mkubwa unahitajika kutoka kwa wananchi na jamii kwa ujumla, kuanzia ngazi ya familia na kwamba tayari wametoa mwongozo ambao ulizinduliwa Julai 2, 2022 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.