Watuhumiwa kuweka sumu vyanzo vya maji

WAFUGAJI katika kijiji cha Kaloleni, kata ya Ubena, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani wamewatuhumu wakulima kuweka sumu katika vyanzo vya maji ikiwemo malambo ya kunyweshea mifugo hatua ambayo inahatarisha usalama wao.

Hayo yalibainishwa leo na wananchi hao wakati wakizungumza katika mkutano wa adhara wa mbio za Bendera wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo ambapo walisema kumekuwa na sintofahamu baada ya sumu kumwagwa katika vyanzo vya maji.

Ramadhani Rashidi alisema watu ambao wanasadikiwa kuwa ni kundi la wakulima wamekuwa wakimwaga sumu katika vyanzo vya maji kutokana na kuwepo kwa migogoro baina yao na wafugaji kutokana na mashamba yao kuvamiwa na mazao kuharibiwa

“Hatuna amani katika kijiji chetu cha kaloleni, kundi la watu ambao wanadhaniwa ni wmwakulima wamekuwa wakimwaga sumu katika vyanzo vya Maji …hii ni hatari Kwa usalama wetu na yote haya ni kutokana na mgogoro baina yetu maana wafugaji wanaingiza mifugo mashambani kwetu wanakula na kuharibu mazao. “alisema

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Lukas Sultan, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo alisema tayari sampuli za maji kutoka katika vyanzo hivyo zimechukuliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo zaidi ili kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo.

Diwani kata ya Ubena, Geofrey Kamugisha, alikiri kuwepo suala hilo na kwamba tayari vyombo vya usalama vipo katika kijiji hicho kudhibiti na kwamba watakao bainika hatua Kali za kisheria zitachukuliwa.

“Vyombo vya usalama vipo na vinafanyakazi ya kudhibiti hali hiyo lakini suala kubwa hapa lile eneo lilitegwa kwa ajili ya malisho lakini limevaniwa hivyo mgogoro ni kati ya wafugaji na wakulima, tunategemea kupata eneo jingine kwa ajili ya malisho na amini tukipata mgogoro huo utamalizika”alisema

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Bagamoyo CCM, Abdurashidi Zahoro, aliagiza viongozi hao kuhakikisha wanatatua mgogoro huo Kwa wakati kabla ya madhara zaidi kutokea ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote walihusika.

“Nimeshtushwa na suala la kuwekwa sumu kwenye vyanzo vya maji ni jambo la hatari sana niagize viongozi wote hususani diwani kukutana na pande zote mbili na kukaa nao ili kuwasulihisha na uchunguzi ufanyike na watakao bainika hatua Kali zichukuliwe.”amesema

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button