Watumia njia za uzazi waongezeka 150% Nzega

NZEGA, Tabora: MATUMIZI ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango yameongezeka katika Zahanati ya Ubinga, Kijiji cha Ubinga wilayani Nzega mkoani Tabora ambapo kwa sasa wanahudumia wahitaji 100 kwa mwezi, kutoka wahitaji 40 mwaka 2021 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 150.

Wakati kukiwa na ongezeko hilo, mkakati wa serikali katika matumizi ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2019/2023 ulikuwa unakadiriwa kupunguza mimba zisizotarajiwa 7,148,748, utoaji mimba holela 2,669,638 na vifo 22,164.

Pia, Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) wa 2030 ni utambuzi wa upatikanaji wa huduma za afya ya ngono na uzazi kwa wote.

Uwekezaji wa makusudi na endelevu katika huduma za upangaji uzazi ni muhimu katika mlingano huu. Moja ya kanuni elekezi ya maono ya FP 2030 ni kuwawezesha wanawake na wasichana na kuwashirikisha wanaume na wavulana.

Maono hayo yanabainisha: “Ujumuisho mzuri wa wanaume unahitajika ili kubadilisha kweli uhalalishaji wa upangaji uzazi,”

Soma pia: https://habarileo.co.tz/uzazi-wa-mpango-utakupa-raha-utaepuka-karaha/

Aidha, ongezeko hilo la matumizi ya uzazi wa mpango katika kijiji hicho cha Ubinga umetokana na uhamasishaji uliofanywa na Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) la Maria Stopes Tanzania katika mradi wake wa kuimarisha vituo vya umma (Public Sector Streghtening-PSS) kuwawezesha wahudumu wa afya kupata elimu na kuwajengea uwezo na kuwezesha upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango.

Akizungumza na HabariLeo, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ubinga, Raphael Peter amesema mafunzo yaliyotolewa na Maria Stopes yameleta tija kwa jamii yao.

Amesema, tangu wahudumu wapate mafunzo ya utoaji huduma wa uzazi wa mpango na kuwezeshwa vifaa, huduma hizo zimekuwa zikifanyika kila siku katika zahanati hiyo tofauti na hapo mwanzo ambapo huduma zilifanyika mara moja kwa mwezi.

“Siku za nyuma huduma hizi hazikutolewa kwasababu watoa huduma walikuwa hawana ujuzi huu vizuri, kwahiyo tulianza kuhamasisha kupitia wahudumu wetu waliopo kwenye jamii wateja wakaanza kuongezeka namba iliongezeka na zaidi namba hiyo inajieleza kwenye vitabu kulingana na takwimu zilizopo kwenye mifumo ya afya,” amesema Dk Peter.

Soma pia: https://www.instagram.com/p/C7MVzwROW6i/?utm_source=ig_web_copy_link&igsh=MzRlODBiNWFlZA==

Amesema kituo cha Ubinga kimenufaika kwa kiwango kikubwa kwa kupata vitendea kazi vya mara kwa mara na kutembelewa na wadau wengi hivyo kufanya huduma za uzazi wa mpango kuwa hai huku akitaja changamoto kubwa kuwa ni kuwa na muitikio mdogo kwa upande wa akina baba.

Kwa upande wake Muuguzi na Mkunga katika zahanati ya Ubinga Aziza Simangwa amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya imani potofu ambapo zinaletwa na maneno ya mtaani na kupotosha watu kuhusu uzazi wa mpango.

Habari Zifananazo

Back to top button