Watumia Sh mil.456 kutokomeza malaria
HALMASHAURI ya Wilaya ya Geita (Geita Vijijini) imetumia kiasi cha Sh milioni 456.
64 kati ya mwaka 2017 hadi 2023 kutekeleza mradi wa kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
Mratibu wa Udhibiti Malaria Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Gabriel Wangese ameeleza hayo mbele ya viongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa walipotembelea zahanati ya kijiji cha Chigunga .
Amesema fedha hizo zimetumika kununua vyandarua 892,223 vilivyogawiwa bure kwa wazee, wajawazito, watoto na watu waishio na virusi vya Ukimwi kati ya mwaka 2017-2022 na vyandarua 45,664 vilivyotolewa hadi Mwezi Mei, 2023.
Amebainisha mradi huo wa ugawaji wa vyandarua ni kielelezo cha njia mojawapo ya kudhibiti mbu waenezao malaria unaofanyika katika vituo 61 vinavyotoa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa makundi maalumu.
Amesema mbali na ugawaji wa vyandarua pia mikakati mingine ya kukabiliana na malaria imetekelezwa ikiwemo unyunyiziaji wa dawa ya ukoko majumbani pamoja na uchunguzi na utambuzi wa malaria kwa vipimo sahihi.
“Hiyo imepunguza kiwango cha vifo vitokanavyo na malaria kwa kila watu 100,000 kutoka asilimia 9.8 hadi asilimia 4.5 na kupunguza wagonjwa wanaolazwa kutoka asilimia 48.8 mwaka 2018 hadi asilimia 33.6 mwaka 2022.”
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita kuhakikisha wananchi wanabaki salama dhidi ya malaria na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023 amegawa vyandarua 100 kuunga mkono juhudi za kudhibiti malaria huku akisisitiza matumizi sahihi ya vyandarua ili kufanikisha kampeni ya ‘Ziro Malaria Inaanza na Mimi’.