MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA), imezitaka kampuni pamoja na watumiaji wa kemikali ya zebaki kuhakikisha wanajisajili Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na nyumbani hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo na Mkemia mkuu wa Serikali Dk Fidelice Mafumiko, wakati wa mkutano na wandishi wa habari mkoani Mwanza.
‘’Hadi kufikia tarehe ya leo, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, inazitambua kampuni 10 ambazo zimekidhi vigezo na matakwa ya sheria na kusajiliwa,’’ amesema Dk. Mafumiko.
Aliwaelekeza wadau wote wanaojihusisha na zebaki ikiwemo watumiaji ambao hawajasajiliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wafuate taratibu za sheria na kanuni katika ununuzi, uuzaji, utumiaji na usambazaji wa kemikali hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Jema Chemicals, Fredrick Otieno ameiomba ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali iendelee na mikakati mbalimbali ya utoaji elimu kuhusiana na matumizi ya kemikali aina ya zebaki.