Watumiaji mto Ruvu wawekwa hadharani

BODI ya Maji Bonde la Wami Ruvu imeeleza ya kwamba kiasi cha maji yanayochukuliwa na wadau katika Mto  Ruvu unaotokana na vyanzo vya safu ya Milima ya Uluguru ni mita za ujazo milioni 1.6 kwa siku.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji bonde hilo, Mhandisi Elibariki Mmassy amesema hayo kwenye kikao kazi ilichokutanisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Morogoro wakiongozwa na mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Rebeca Nsemwa.

Kikao hicho kilikuwa cha kuainisha majukumu ya bodi hiyo na pia kutumia fursa hiyo kuiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya kazi kwa kushirikiana na bodi katika  maeneo yenye changamoto ya uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo aliwataja wadau wakubwa wanaotumia maji ya mto Ruvu ni Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa mita za ujazo 590,000 kwa siku, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), mita za ujao 61,500 kwa siku na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), ni mita za ujazo 34,000 kwa siku.

Mhandisi Mmassy ametaja matumizi ya maji kitaasisi kwenye mabano ( Mzinga, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Chuo Kikuu Mzumbe na Mlali) ambazo kwa ujumla ni mita za ujazo 2,013 kwa siku.

Kwa upande wa mahitaji ya umwagiliaji na ufugaji wa samaki matumizi ni mita za ujazo 216,518 kwa siku na kwenye uhifadhi viumbe hao na mazingira mita za ujazo 775, 008 kwa siku.

Mhandisi Mmassy pia amesema bodi hiyo hadi  kufikia Juni 2023  ilitoa vibali vya matumizi ya maji 410 kati ya 2,477 sawa na asilimia 16.6  na idadi ya vibali vya kuchimba visima 529 kati ya 921 sawa na asilimia 57.4.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button