Watumishi 22,112 kuajiriwa afya, elimu
DODOMA; SERIKALI imesema katika mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 22,112 wakiwemo wa afya 10,112 na elimu 12,000, ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu mkubwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chunya, Masache Kasaka aliyehoji ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kada ya afya na elimu katika Wilaya ya Chunya.
“Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada za elimu na afya kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Kati ya mwaka 2020/21 na 2022/23, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ilipokea jumla ya watumishi 397 wakiwemo wa afya 84 na elimu 313 ambapo walimu wa shule za msingi walikuwa walimu 244 na shule za sekondari walikuwa 69.
“Katika mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 22,112 wakiwemo wa afya 10,112 na elimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Wilaya ya Chunya,” amesema Naibu Waziri.