Watumishi Mafinga watuhumiwa kunufaika na mkopo sugu

WALIOKUWA wajasiriamali wanachama wa kikundi cha Mnyigumba kilichokuwa na kiwanda kidogo cha kuzalisha sabuni mjini Mafinga wilayani Mufindi wamekalia kuti kavu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego kuagizwa wakamatwe.

Kikundi hicho kilichokuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa wajasiriamali wadogo wa halmashauri ya Mji Mafinga baada ya kuanzisha kiwanda hicho kimeingia katika msukosuko huo ikiwa ni matokeo ya kushindwa kukamikisha kulipa zaidi ya Sh milioni 93 kilichokopeshwa na Halmashauri ya Mji Mafinga.

Taarifa iliyotolewa katika baraza maalumu la halmashauri hiyo lililojadili na kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha kati ya deni hilo walilokopeshwa mwaka wa fedha 2018/2019, kikundi hicho chenye wanachama zaidi ya 10 kimefanikiwa kulipa Sh milioni 18 tu.

Akichangia kuhusu hoja hiyo Diwani wa Kata ya Isalavanu, Charles Makoga alisema wapo baadhi ya viongozi na watumishi wa halmashauri hiyo waliojipenyeza katika kikundi hicho na kujinufaisha na mkopo huo.

Ili iwe fundisho kwa viongozi na watumishi hao, Makoga aliitaka serikali pamoja na halmashauri yao kulifuatilia suala hilo kwa kina na kuchukua hatua kali ili walipe deni hilo.

“Kuna watu wawili wawili kutoka katika baadhi ya kata waliingizwa katika kikundi hicho lakini sio waliokopa mkopo huo. Waliokopa na kuutumia ndivyo sivyo ni baadhi ya viongozi wa halmashauri hii na serikali, na walipoona mambo yanaanza kuwa magumu wakaanza kuwaingiza watu hao ili kuzugia lakini watu hao hawajui chochote kuhusu mkopo huo kwasababu wao siyo waliokopa,” alisema Makoga.

Akitoa maelekezo ya kukamatwa kwa wanakukindi hao, Dendego alisema; “Wasakwe popote waliopo, wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya dola.”

Alisema hata kama wapo baadhi yao waliofariki aliitaka halmashauri hiyo kutumia sheria kukamata dhamana zao walizotumia kupata mkopo huo na kuziuza ili kufidia kulipa fedha hizo za walipa kodi.

“Ukifuatilia kwa kina suala hili kuna viashiria vya uwepo wa nia ovu ya kuiibia serikali wakati kikundi hicho kikikopeshwa fedha hizo. Nawaagiza wakuu wa idara kuweni waadolifu, wazalendo na wakali mnaposimamia rasilimali za umma,” alisema.

Katika kulishugulikia suala hilo kwa wakati, Dendego ameiagiza halmashauri hiyo kumpatia majina ya wahusika wote wakiwemo waliokuwa viongozi wa kikundi hicho ambao ni pamoja na Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina ili wabanwe vilivyo na kurejesha fedha hizo.

Akisisitiza ukusanyaji wa madeni ya halmashauri, Dendego aliwataka madiwani kujiweka kando na fedha za serikali kwa kutoleta siasa na kutoa ushirikiano pale wanapobaini kuna vikundi hewa katika kata zao vinavyonufaika na mikopo mbalimbali inayotolewa na serikali.

Akihitimisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Reginald Kivinge mbali na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuhudhuria katika kikao hicho lakini pia amewaahidi yeye pamoja na madiwani wataendelea kusimamia halmashauri hiyo kwa kushirikiana na watumishi ili kuleta maendeleo zaidi na hawatasita kuchukua hatua pale taratibu zitakapokiukwa.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa hoja nyingi za CAG kwenye halmashauri hiyo ni suala la uzembe wa baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wakiwemo maafisa maendeleo wa kata na watendaji kwa kutokuwa makini katika majukumu yao na kuagiza wabadilike na kuwajibika ipasavyo ili kusijitokeze hoja zinazotokana na uzembe.

Katika ripoti ya CAG inaonesha halmashauri ya Mji Mafinga ilikuwa na jumla ya hoja 25 ambazo kati yake 10 zimeshatatuliwa na kufungwa huku 15 zikiwa bado katika hatua ya utekelezaji hali iliyopekea halmashauri hiyo kupata hati safi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x