‘Watumishi msiwe waoga kueleza changamoto zenu’

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi, amewataka watumishi wa umma nchini, kutoogopa kutoa malalamiko yao na kueleza changamoto zao kwa viongozi wao, ili kuweza kutatuliwa na kuacha  woga, kwani Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mpenda haki.

Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kuzungumza na watumishi wa umma katika Manispaa ya Wilaya ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.

Akizungumza na watumishi hao, Naibu Waziri Ndejembi amewataka kuacha woga wanapoona viongozi wa kitaifa wamewatembelea, badala yake waeleze changamoto zinazowakabili, ili ziweze kutatuliwa.

” Ofisi ya Rais Utumishi kwa kutambua thamani ya watumishi wa umma, ndio maana tunafanya ziara za kuja huku chini kuwasikiliza nyinyi ambao ndio watoa huduma na watendaji wa serikali kwa wananchi huku chini.

“Niwaombe msiogope elezeni changamoto zenu na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia, ipo tayari kuzitatua zote, lengo ni kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwenye mazingira bora.

“Niwaase pia kuheshimiana kwenye maeneo yenu ya kazi, mkubwa amheshimu mdogo na mdogo amheshimu mkubwa, wote hapa mmekutanishwa na kazi, kazi ya kuwatumikia Watanzania, serikali haitotaka kuona kuna makundi kwenye maeneo ya kazi, wote mna jukumu la kumsaidia kazi Rais Samia katika kuwatumikia Watanzania.

“Niwasihi kuacha fitna, chuki na vita kwenye maeneo ya kazi, sisi watumishi wa umma ndio wenye jukumu la kuhakikisha tunamsaidia Rais wetu kutekeleza na kusimamia miradi hii mingi na mikubwa inayoletwa kwenye Halmashauri zetu,” amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Amewataka watumishi wa umma Mkoa wa Lindi kujituma na kufanya kazi kwa weledi, ikiwa ni pamoja na kutumia taaluma zao kuhakikisha Mkoa huo unakua kiuchumi.

” Lindi ya leo siyo ya miaka ya nyuma, Rais wetu ameifungua nchi yetu ndani na nje ya mipaka yetu, leo mkoa huu unafunguka na fursa zinakuja, LNG inakuja, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kinafungua tawi lao hapa, Chuo cha Ufundi Arusha hivyo hivyo.

“Nyinyi kama watumishi wa umma mna wajibu wa kuisaidia serikali yenu kuonesha jinsi gani Lindi sasa inakua na fursa ni nyingi, ili wawekezaji waje kuwekeza hapa,” amesema Ndejembi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button