Watumishi Mwanza wahimizwa ubunifu kwenye kazi
KATIBU Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amewataka watumishi mkoani humo kuwa wabunifu kwenye kazi bila kusubiri kuelekezwa kutoka kwa wakuu wa idara na viongozi wao juu ya nini cha kufanya ili kupata matokeo mazuri.
Ametoa wito huo kupitia kikao alichokifanya leo Desemba 2, 2025 na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambacho kilikua na lengo la kukumbushana majukumu ya kazi.
SOMA: RC Mtanda: Miradi ya Trilioni 5.6 yatekelezwa Mwanza
Aidha Balandya amesema katika kufanikisha hilo watumishi katika idara zao wanatakiwa kushirikiana na kufanya kazi kwa ubunifu na ueledi ili kuunganisha taasisi nzima katika kuleta tija kwenye utendaji na kwa wananchi.
“Tuwe wabunifu kwenye kazi tutekeleze majukumu yetu yaliyo kwenye muundo wa ajira zetu kwani kila mmoja kwenye eneo lake ana muongozo wa majukumu ya msingi ya kufanya,” amesema Balandya.
Ametoa rai kwa watumishi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kuhakikisha wanaifahamu mifumo mbali mbali ambayo imewekwa ili kusaidia uharakishaji na ufanisi wa majukumu katika ofisi.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Mwanza amewasihi kuilinda amani ya nchi na kuchukua tahadhari kwenye makazi yao wanapoishi.



