Watumishi Tanapa kupewa mafunzo ya kijeshi

MWENYEKITI Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Generali Mstaafu, George Waitara amesema muda umefika kwa shirika hilo watumishi wake kwenda katika mafunzo ya kijeshi kwani kwa muundo wa sasa hauruhusu kufanya kazi ukiwa raia.

Waitara alisema hayo Agosti 22, 2023 jijini Arusha mara baada kukabidhi nyaraka za utendaji kazi akiwa Mwenyekiti wa Tanapa kwa zaidi ya miaka sita na kusema kuwa zamani watendaji na wafanyakazi wa Tanapa walikuwa na sharubu lakini baada ya kuingia katika mfumo kila mmoja anafanyakazi kwa kufuata misingi ya kijeshi.

Alisema kutokana na hali hiyo amewataka wafanyakazi wote wa Tanapa na watendaji kujiandaa kwenda katika mafunzo ya kijeshi ili wajue wajibu wao katika kutenda kazi na kujua maana halisi ya uzalendo na kuheshimu mipaka ya kazi.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa bodi ilikuwa ikifanya kazi kwa makubaliano ya pamoja na menenjimenti ya shirika hilo na hoja zilikuwa zikijadiliwa na sio mtu, watu au bodi haikuwahi na haitawahi kuigawa menejimenti katika kipindi cha miaka yote ya uenyekiti wake.

Alisema kuwa hali hiyo itakuwa hivyo katika kipindi kijacho lengo ni kutaka kila mmoja awajibike katika nafasi yake kwa maslahi ya taifa na sio vinginevyo.

‘’Watendaji na wafanyakazi wote wa Tanapa wanapaswa kwenda katika mafunzo ya kijeshi kwani huwezi kuwa katika mfumo wa kijeshi na hujaenda jeshini hilo haliwezekani.

’’alisema Waitara.

Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Balozi, Dk Ramadhani Dau pamoja na kumshukuru Rais samia kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo aliwataka wafanyakazi na watendaji wa TTB kuhakikisha wanajituma na kufanyakazi kwa maslahi ya nchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii nje ya nchi ili malengo ya serikali yanafikiwa kwa asilimia 100.

Balozi Dau alisema wakati umefika wa TTB kujikita katika kutangaza utalii katika Bara la Asia kwa kuwa ni Bara lenye watu wengi duniani na kusema kuwa kama hilo likifanikiwa huenda idadi ya watalii milioni 5 hadi kufikia mwaka 2025 ikafikiwa.

Alitolea mfano nchi ya Singapore kuwa mwaka 2018 ilifanikiwa kuingiza mapato ya Dola bilioni 21 kwa kuingiza watalii katika nchi kuwa ni ndogo kuliko Zanzibar na kwa nini Tanzania inashindwa kufikia malengo wakati ina vivutio vingi kuliko Singapore.

Balozi Dau alisema Mapato hayo kwa hapa Tanzania ni Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii na chenji inabaki hivyo wakati umefika wa TTB kujikita katika Bara la Asia kutangaza Utalii.

Alisema analijua vizuri Bara la Asia kwa kuwa ameishi huko kwa zaidi ya miaka saba hivyo ana amini kuwa upo uwezekano wa watalii kuongezaka na nchi kuingiza mapato zaidi iwapo kutakuwa na uwajibikaji wa pamoja.

Habari Zifananazo

Back to top button