Watumishi wa umma waonywa utoro sikukuu

Watumishi wa umma waonywa utoro sikukuu

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini, kuacha tabia ya kutoroka kazini katika kipindi hiki cha sikukuu na badala yake wafuate taratibu za uombaji wa likizo.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo, wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, ambapo ameanza ziara yake ya kuzungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema katika kipindi hiki cha sikukuu ipo tabia ya baadhi ya watumishi kutaka kwenda kusherehekea sikukuu, bila kufuata taratibu za kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kuomba likizo au kuwa na ruhusa ya kutoka katika vituo vyao vya kazi na hali hii inasababisha wananchi wengi  kukosa huduma wanayostahili.

Advertisement

” Najua tupo mwisho wa mwaka na kuna sikukuu kadhaa, wapo watumishi ambao wanapanga kutoroka kwenda kusherehekea, niwasihi kuacha tabia ya kutoroka na badala yake mfuate taratibu zote za kuomba likizo, mnavyotoroka mnawaumiza Watanzania wengine wanaohitaji huduma.

“Sisi watumishi wa umma ni watoa huduma wa serikali kwa wananchi wetu, na serikali huwa haiendi likizo, hata kipindi hiki cha sikukuu bado Watanzania wanahitaji kuhudumiwa na serikali yao.

“Hatutegemei kuona watu mnatoroka maofisini kwenda kula sikukuu bila kuwa na likizo au ruhusa na kuacha Watanzania wenzetu wakihangaika kutafuta huduma kwenye Ofisi za umma,” amesema Ndejembi.