Watumishi wa umma washauriwa uwekezaji kabla ya kustaafu

WATUMISHI wa umma mkoani Tabora wameshauriwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara kwa kutumia fursa za mikopo zilizopo ili watakapostaafu wawe na vyanzo vingine vya mapato.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Batilda Buriani alipokuwa akifungua warsha ya siku moja ya walimu na kuzindua Kifurushi cha NMB Mwalimu Spesho –umetufunza, tunakutunza iliyofanyika juzi mjini hapa.

Alipongeza benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha walimu na watumishi wa sekta nyingine kujikomboa kiuchumi kabla na baada ya kustaafu.

Alibainisha lengo la taasisi hiyo kuwa ni kuona watumishi wa umma wakianzisha miradi itakayowaongezea kipato na kujiimarisha zaidi kiuchumi kupitia mikopo hiyo yenye riba nafuu na isiyo na masharti ili kuboresha maisha yao.

Balozi Batilda aliipongeza kwa kuandaa siku maalumu ya walimu ikiwa ni moja ya mkakati wao wa kufikia walimu zaidi ya 5,000 chini ya Kauli mbiu ya Mwalimu Spesho, umetufunza tunakutunza.

Awali Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magese aliwataka walimu na watumishi wengine wa umma kufika tawi lolote la benki hiyo wanapokuwa na changamoto zozote za kifedha ili kuzipatia ufumbuzi.

Alisema wamewaita katika warsha hiyo kama wadau kwa ajili ya kutafuta maoni yao ambayo yatatumika kuboresha utoaji huduma kwa wateja wao.

Naye Meneja Mwandamizi wa benki hiyo, Ally Ngingite alisema lengo la warsha hiyo ni kuwapa walimu elimu ya kifedha ili wapate uelewa wa kupanga matumizi ya fedha wanazopata ikiwemo mikopo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button